Saturday 20 May 2017

HAKI MADINI KUANDAA MDAHALO



Wachimbaji wadogo wa madini, wachuuzi na madalali wa madini nchini wanatarajia kufanya mdahalo wa kitaifa juu ya umuhimu wa sekta ya madini na namna ya kuwanufaisha zaidi.

Mkurugenzi wa shirika la Haki Madini Amani Mhinda, akizungumza mji mdogo wa Mirerani na viongozi wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema) alisema mdahalo huo utafanyika mkoani Geita.

Mhinda alisema lengo la mdahalo huo ni kuwaleta wadau mbalimbali kwa pamoja ili kuzungumzia changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa wachimbaji wadogo na kutafakari kitaifa maono ya wachimbaji.  

Alisema wanatarajia kufanya mdahalo huo mwishoni mwa mwezi Juni kwa kushirikiana na shirika kiongozi duniani la maendeleo la International Institute for Environment and Development (IIED).



“Haki madini tunarajia mpango huu utatoa jukwa hitajika kwa wadau kushirikiana na kubadilishana ujuzi na kukuza utawala bora kuwa sauti kubwa, usalama na utengenezaji,” alisema Mhinda.

Alisema uchimbaji mdogo wa madini unaweza kutoa mchango chanya wenye umoja na usawa wa maendeleo endelevu na ukuaji wa uchumi, kwani husaidia mamilioni ya watu hasa wanawake na watoto.

Katibu wa Marema Tawi la Mirerani, Abubakari Madiwa alisema kupitia mdahalo huo wanatarajia wachimbaji mdogo kunufaika kwa kujengewa uwezo hivyo wamejiandaa kushiriki mara utakapofanyika.

“Haki madini imekuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji madini wadogo kwani tumekuwa pamoja bega kwa bega kwa kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata haki zao,” alisema Madiwa.

No comments:

Post a Comment