Tuesday, 6 June 2017

WAFUGAJI WALIA NA UCHACHE WA VYUMBA VYA MADARASA NA WALIMU



Wanafunzi wa shule ya msingi Lesirwai, Kijiji cha Marwa Kata ya Ruvu
Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro, wanakabiliwa na changamoto ya kusoma madarasa mawili wakitumia chumba kimoja.

Kutokana na uhaba wa madarasa, wanafunzi wa madarasa ya kwanza na la pili, la tatu na la nne, la tano na la sita, husoma kwenye chumba
kimoja huku wale wa darasa la saba wakitumia ofisi ya walimu.

Wakizungumza shuleni hapo, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho
walidai kuwa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2014 ina wanafunzi wa
darasa la kwanza hadi la saba ila ina vyumba vinne tuu vya madarasa.

Mmoja kati ya wananchi hao,  Zacharia Leyani alisema japo kuwa jamii ya eneo hilo hivi sasa ina mwamko mkubwa lakini wanakwamishwa na miundombinu mibovu ya shule hiyo.

Alisema wanafunzi wanakuwa na wakati mgumu wa kufuatilia masomo kwa usahihi kwani wanakuwa wanafuatilia mafundisho mengine pindi wenzao wakiwa wanafundishwa na mwalimu.

“Chumba kimoja cha darasa hivi sasa wanafundishwa wanafunzi wa
madarasa mawili sasa sijui mwalimu atakuwa na mwamko gani wa
kufundisha tunaomba serikali iangalie hii hali,” alisema Leyani.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Tendwa Barnaba alithibisha wanafunzi hao kusoma kwenye chumba cha darasa moja kutokana na uhaba wa madarasa uliopo huku wanafunzi wa darasa la saba wakitumia ofisi .

Barnaba alisema pamoja na uchache wa vyumba vya madarasa, pia shule hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu kwani japokuwa kuna wanafunzi 140 wapo walimu watatu pekee.

“Changamoto hizo zingepatiwa ufumbuzi tungepata moyo, tunaomba
tuongezewe vyumba vya madarasa na walimu, kwani mwalimu mmojaanafundisha takribani masomo 10 kwa siku moja,” alisema.

Hata hivyo, ofisa tawala wa wilaya ya Same, Sospeter Magonera alisema uchache wa madarasa ni changamoto ya shule hiyo na kupitia bajeti ya halmashauri wanatarajia kutenga fedha ili yajengwe.

Magonera anasema serikali inatoa kipaumbele kwenye shule za pembezoni ila watawashirikisha jamii ya eneo hilo ambayo ina utajiri wa mifugo ichangie ujenzi ili serikali iiunge mkono kuliko kuiachia serikali
pekee.

“Suala la walimu nalo litapatiwa ufumbuzi kwani hivi karibuni kuna
ajira mpya za walimu 52,000 zilizotengwa na tunatarajia wale wa Same baadhi yao watapangiwa shule hii,” alisema Magonera.

No comments:

Post a Comment