Thursday, 13 October 2016

WANYONGE KULIPIWA MATIBABU YA iCHF HANANG'


Wananchi wanyonge ambao ni kaya masikini wamenufaika baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, George Bajuta, kujitolea sh1.8 milioni kwa ajili ya kuzilipia kaya masikini 36 za watu 216 wa Kata ya Simbay kwenye mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa (iCHF).

Bajuta ambaye ni diwani wa kata hiyo aliyasema hayo kwenye uzinduzi wa mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa (iCHF) ulioandaliwa na mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoani humo na kudai kuwa kila kitongoji kitatoa kaya tatu za wanyonge wasiojiweza.

Alisema kata yake ina vitongoji 12 na kila kitongoji kitachagua kaya tatu ambazo ni familia za wanyonge zisizojiweza ili awalipie sh30,000 kila kaya yenye watu sita, baba, mama na watoto wanne, zitakazopata huduma za afya kwa mwaka mzima.

“Mimi sina utajiri mkubwa ila nimeamua kujitolea kidogo nilichonacho kwa kuhakikisha wale ndugu zangu wanyonge wasiokuwa na uwezo kabisa kwenye kila kitongoji nao wapate fursa ya kutibiwa bure kwa mwaka,” alisema Bajuta.


Mkuu wa wilaya hiyo Sarah Msafiri akizungumza wakati akizindua mfuko huo alisema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kushiriki ipasavyo kwa kujiunga na (iCHF) kwani hadi mwisho wa mwaka inatakiwa asilimia 50 ya watu wajiunge.

“Hapa kwenye Tarafa ya Simbay kuna zaidi ya wakazi 6,200 hivyo tunapaswa kujiunga kwa wingi ili watu zaidi ya 3,100 ambayo ndiyo nusu ya watu ili kutimiza lengo la serikali la kuhakikisha hadi idadi hiyo inafika,” alisema Msafiri.

Meneja wa mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoani Manyara, Isaya Shekifu alisema kila kaya itakayotoa sh30,000 kwa ajili ya kuchangia mfuko huo nayo serikali kuu huchangia nusu nyingine sh30,000 na kuwa sh60,000.

Shekifu alisema iCHF iliyoboreshwa inajenga mfuko endelevu wa kuchangia kijamii gharama za matibabu na kuboresha ubora wa huduma za afya kupitia mafunzo kwa watoa huduma, utoaji vifaa tiba na uboreshaji miundombinu ya huduma.

No comments:

Post a Comment