Thursday, 13 October 2016

CRDB YATOA MIKOPO YA SH16.1 BILIONI MKOANI MANYARA

Benki ya CRDB Tawi la Babati Mkoani Manyara, imefanikiwa kutoa mikopo ya sh16.1 bilioni kwa wajasiriamali, watumishi wa Serikali, watumishi wa sekta binafsi, vyama vya kuweka na kukopa na asasi za fedha.

Watumishi wa serikali na wasekta binafsi 1,604 walikopeshwa sh12.8 bilioni na wajasiriamali 84 walikopa sh3.3 bilioni ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara na wakulima.

Meneja wa benki ya CRDB Tawi la Babati, Ronald Paul akizungumza kwenye kilele cha wiki ya huduma kwa wateja, alisema wamedhamiria kuwapa wateja wao huduma bora na kuwanyanyua kiuchumi.

Paul alisema kwa muda wa miaka miwili tangu waanzishe huduma ya benki hiyo mkoani Manyara, wamefanikiwa kufungua matawi mengine madogo wilaya za Mbulu, Hanang, Simanjiro na Kiteto.

Alisema pia wamefanikiwa kufungua huduma za matawi madogo yaliyopo Magugu, Haydom na Mirerani ambayo kupitia hayo wameweza kupata akaunti za halmashauri za wilaya.

Alisema kwenye matawi yao madogo wamefanikiwa kuwa na huduma za ATM ambazo wamefungua 10 kwenye mkoa huo na zinafanya kazi kwa muda wa saa 24.

"Kwa kipindi hiki tumefanikiwa kuongeza ajira kwa watanzania hususani kwa wana Manyara kutoka wafanyakazi 12 hadi 37 kutokana na matawi mengine madogo yaliyofunguliwa katika wilaya mbalimbali," alisema.

Alisema wamefanikiwa kupata amana za sh11 bilioni zilizotokana na wateja 12,000 waliofungua akaunti za akiba, watoto jumbo, akaunti za malkia, akaunti maalum, bidhaa nyingi za kibenki za Simbanking, ATM na fahari huduma.

Mkurugenzi wa mji wa Babati Fortunatus Fwema alitoa wito kwa benki hiyo kuwatafutia wateja wa mbaazi wa nje ya nchi kwani hivi sasa wakulima wengi wanapata changamoto ya soko la zao hilo.

Fwema alisema kutokana na benki hiyo kutoa huduma za fedha hadi nje ya nchi hasa nchini India, wangetumia fursa hiyo kwa kuwaunganisha wakulima hao moja kwa moja na soko la mbaazi ambalo wanunuzi wengi hutoka nchini India.

No comments:

Post a Comment