Benki ya CRDB imetoa msaada wa mashuka 100 kwenye hospitali
ya rufaa ya Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, kwa lengo la kuwasaidia
wagonjwa wanaolazwa katika hospitali hiyo inayohudumia zaidi ya watu wa mikoa minne
nchini.
Akizungumza wakati akikabidhi mashuka hayo 100 kwa
mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk Emanuel Nuwass, Meneja wa CRDB Tawi la Babati
Ronald Paul alisema wanatoa msaada huo ili kurudisha hisani kwa jamii.
Paul alisema wamekabidhi mashuka hayo ili kutoa asante kwa jamii
kwenye wiki ya huduma kwa wateja, kwa kurudisha kwao kile kidogo wanachopata
kwa ajili ya kuboresha mahusiano zaidi baina ya benki hiyo na wateja wake.
“Tutaendelea kushirikiana na kusaidiana kwenye masuala
mbalimbali ya kijamii kwani tunatambua jitihada na changamoto ya hospitali ya
Haydom ambayo inatoa huduma kwa watu wa Manyara na waliopo mikoa ya jirani,”
alisema.
Hata hivyo, mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk Emanuel Nuwass
alisema hii ni mara ya tatu kwa benki hiyo kutoa msaada kwenye hospitali ya
Haydom, hivyo iendelee kuwa karibu nao kwa ajili ya kupeana ushirikiano wa
kusaidia jamii.
Dk Nuwass alisema awali benki hiyo ilitoa mchango wa
maendeleo wa sh1 milioni kwa ajili ya siku ya Haydom, kisha wakawapa zawadi ya
ng’ombe mmoja mkubwa wa siku ya familia na mashuka 100 yatakayotumiwa na
wagonjwa.
Alisema hivi karibuni bodi ya hospitali hiyo ilikubaliana na
mpango wa malipo kwa wagonjwa kupitia njia ya kadi ya CRDB na zoezi hilo
linatarajia kuwarahisishia watu wote watakaopata huduma katika eneo hilo la
Haydom.
Kwa upande wake, meneja masoko mwandamizi wa benki hiyo
Fredrick Siwale alisema benki hiyo itandelea kutoa huduma nzuri kwa wateja wao
huku ikiboresha maeneo ambayo huduma haipatikani kwa kuhakikisha wanakuwepo.
“Kupitia kauli mbiu yetu ya ulipo tupo kama hatupo tutakuja
na kama hatujaja utusubiri, tunalenga kuwahudumia watanzania wote na kupitia
hilo ndiyo sababu tukafika kutoa mashuka haya kwani tunaithamini jamii,”
alisema Siwale.
No comments:
Post a Comment