Benki ya CRDB Mkoani Manyara, imetoa msaada wa madawati 200 kwa
halmashauri ya mji wa Mbulu kwa ajili ya kutumika kwenye shule za msingi, kwa lengo
la kuhakikisha tatizo la madawati linamalizika katika eneo hilo.
Akizungumza wakati akikabidhi madawati hayo, meneja wa
CRDB Tawi la Babati, Ronald Paul alisema katika kuazimisha wiki ya huduma kwa
wateja wamejitolea msaada huo wa madawati hayo 200 kama mchango wao kwa jamii.
Paul alisema benki hiyo ya CRDB imetoa madawati hayo 200
ambayo yatagawanywa kwa wanafunzi wa shule tano za halmashauri ya mji wa Mbulu,
ambapo kila moja ya shule hizo zitatolewa madawati 40.
“Tukiwa kwenye wiki ya huduma kwa wateja tunahakikisha
tunarudisha kile kidogo tunachopata kupitia jamii, sisi tutaendelea kutoa
mchango wetu kwa jamii ili kuhakikisha tunaunga mkono suala zima la maendeleo,”
alisema Paul.
Alisema kwa muda wa miaka miwili tangu CRDB ianze kutoa
huduma zake katika mkoa wa Manyara, wananchi wa mji wa Mbulu wamechangamkia
fursa ya uwepo wao, kwa kuweka fedha, kutoa na kuchukua mikopo ya benki hiyo.
Mkurugenzi wa mji wa Mbulu Anna Mbogo akizungumza wakati
akipokea madawati hayo aliushukuru uongozi wa CRDB kwa kutoa msaada huo kwani
utawasaidia wanafunzi wa shule hizo kusoma kwa ufasaha.
Mbogo alisema awali walikuwa na upungufu wa madawati 3,179
ila walijitahidi na kuhakikisha madawati hayo yanapatikana na hadi sasa wana
madawati 999 ya ziada ambayo yamehifadhiwa kwa ajili ya kutumika baadaye.
Hata hivyo, alitoa ombi kwa CRDB kuendelea kutoa msaada wa
miundombinu ya shule za eneo hilo kwani hivi sasa wana mpango wa kujenga
madarasa mengine ya shule ya msingi Imboru, yenye madarasa mawili pekee.
“Awali wanafunzi wa shule hii walikuwa wanatembea umbali
mrefu wa kilometa tatu kutoka nyumbani hadi shuleni kila siku hivyo ili
kukomesha hali hiyo kwa watoto hawa wadogo ndipo tukaamua kuijenga,” alisema Mbogo.
Alisema lengo lao ni kuhakikisha wanaendelea kuiboresha
shule hiyo mpya kwa kujenga madarasa mengine zaidi ili baada kwani hivi sasa
wanafunzi hao wanapata elimu kwa urahisi kwa sababu ipo karibu na makazi yao.
No comments:
Post a Comment