Wednesday 21 September 2016

WAWILI WANUSURIKA KUFA MGODINI


WACHIMBAJI wawili haramu wamenusurika kufariki dunia baada ya kuishia hewa walipoingia kwa wizi kwenye mgodi wa kampuni ya TanzaniteOne ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Akizungumza na waandishi wa habari, kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi (ACP) Francis Massawe alisema wachimbaji hao haramu waliingia kwenye mgodi wa TanzaniteOne uitwao Investa.

Kamanda Massawe alisema tukio hilo lilitokea juzi alasiri kwenye mgodi huo baada ya wachimbaji hao kuingia kwa wizi chini kwa chini mgodini kupitia mitobozano na kufanya kazi kwenye mgodi huo ambao hautumiwi hivi sasa.


Aliwataja wachimbaji hao haramu ambao walinusurika kufariki dunia kwa kukosa hewa mgodini ni Ramadhani Juma na Mohamed Jumanne wote wakazi wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.

Alisema wanawashikilia watu hao wawili kwa ajili ya mahojiano kabla ya kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma za kuingia kwa jinai kwenye mgodi ambao hawaumiliki wana hawafanya kazi katika mgodi huo.

Hata hivyo, alitoa onyo kwa watu wote wanaowafadhili wachimbaji hao haramu kuzamia bila halali kwenye mgodi wa kampuni hiyo kwani vitendo hivyo huchangia uhalifu kutokana na kufanya kazi eneo ambalo hawalimiliki.


Ofisa uhusiano wa kampuni ya TanzaniteOne Halfan Hayeshi alisema siku ya tukio hilo watu 10 waliingia kwenye mgodi huo wa Investa ambao haufanyiwi kazi kupitia mtobozano uliopo na kuendelea na shughuli zao bila halali.

Hayeshi alisema baada ya kuishiwa hewa kupitia mashine ya jenereta iliyokuwa inatoa hewa ya chafu ya ukaa, watu hao walitoa taarifa kwa mlinzi wa kampuni hiyo ambaye aliwaambia wasubiri atoe taarifa kwa uongozi ndipo wakatoroka.

“Baada ya kufika eneo la tukio tulitoa taarifa polisi na uongozi wa ofisi ya madini Mirerani ndipo tukaanza zoezi la kuwaokoa watu hao ambao tuliwakuta wawili wakiwa na hali mbaya na hadi sasa wanashikiliwa na polisi,” alisema.   

No comments:

Post a Comment