Wagonjwa
wanaopata huduma kituo cha afya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,
wameiomba Serikali kuchukua hatua na kuboresha matibabu kwenye kituo hicho
kwani hivi sasa huduma nyingi zimedorora.
Wakizungumza
kuhusu changamoto hiyo wagonjwa hao walidai kuwa huduma zinazotolewa hivi sasa
kwenye kituo hicho ni vipimo, kliniki ya mama na mtoto na vidonge vya kufubaza
virusi vya ukimwi (ARV) pekee.
Mmoja kati ya
wagonjwa hao John Benarld alisema hivi sasa kituo hicho kina hali mbaya mno
kwani hata dawa zimekuwa tatizo, hadi kusababisha wagonjwa kudhani kuwa wauguzi
wanauza dawa kwenye maduka yao kumbe sivyo.
“Tunaiomba serikali
iingilie kati suala hili kwani ni aibu hata maji ya drip hawana, dawa hakuna
hata paracetamol hazipo na pia hivi sasa ni zaidi ya miezi mitatu maji ya bomba
yamekatika katika kituo hicho cha afya,” alisema Bernald.
Selemani Mohamed
alisema hata upungufu wa watumishi ni tatizo kwani alitumia muda wa saa mbili
kukaa kwenye kiti kwa ajili ya kupata huduma ya vipimo kwenye maabara kutokana
na kuwepo na mtumishi mmoja pekee.
“Nimetoka kwa daktari
muda mrefu na mtoto wangu mdogo anaumwa nimeambiwa niende eneo la maabara akachukuliwe
kipimo cha damu lakini bado sijapatiwa huduma huyu dada yupo peke yake,”
alisema Mohamed.
Alisema kitengo cha
maabara kinapaswa kiwe na wahudumu wawili au watatu kwani kuna wagonjwa wengine
wanafika kituoni hapo wakiwa wana hali mbaya ya kuzidiwa ila hivi sasa kuna
mtaalamu mmoja anayehudumia watu wengi.
Hata hivyo, mganga
mfawidhi wa kituo hicho Dk Raymond Msaki alikiri kuwepo na upungufu wa dawa kwani
wagonjwa wengi wamekuwa wanakosa huduma kutokana na upungufu huo, ila uongozi ulishafikisha
taarifa sehemu husika.
Dk Msaki pia alikiri
kuwepo na tatizo la maji kwenye kituo hicho kwani tangu mwezi Julai maji yaliyounganishwa
na mamlaka ya mji mdogo hayapatikani ila wakitaka maji wanaomba kwa jirani yao kulikokuwa
na shirika la World vision.
“Upungufu wa
watumishi ni kweli kwani sehemu ya maabara hivi sasa kuna dada mmoja yeye ndiye
anaandika wagonjwa anawapima na kutoa majibu, wenzake wawili hawapo, mmoja yupo
masomoni na mwingine yupo likizo,” alisema.
No comments:
Post a Comment