Wednesday 21 September 2016

WAANDISHI WAASWA KUFANYA UTAFIKI HABARI ZA GESI NA MAFUTA


Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia taaluma yao kwa kufanya
utafiti na kuandika ipasavyo habari za mafuta na gesi ili jamii iweze
kutambua namna itakavyonufaika kupitia rasilimali hizo muhimu.


Mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel Daqarro, aliyasema hayo kwenye
mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na
Manyara, yaliyotolewa na shirika la maendeleo ya petrol nchini (TPDC).

Daqarro alisema jamii inapaswa kutambua faida itakazopata kupitia
miradi ya maendeleo ya gesi na mafuta ikiwemo ajira, biashara kwani
mara nyingi wasipopatiwa uelewa hupinga mradi na kusababisha hasara
kwa Taifa.

Alisema suala la bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Uganda nalo
linapaswa kuandikwa kwa marefu na mapana ili wananchi watakaopitiwa na
mradi huo waone faida itakayopatikana kiuchumi kwa wao binafsi na
Taifa kwa ujumla.

Alisema hata zile vurugu za mikoa ya kusini bado kiini chake
hakijalikana ila hivi sasa wananchi wameelewa faida ya gesi ikiwemo
watu wa Mtwara ambao hivi karibuni umeme ulivyosumbua nchini wao
walinufaika na gesi,” alisema .




Kwa upande wake, ofisa habari wa shirika la maendeleo ya petroli
nchini (TPDC) Francis Lupokela, akizungumza na waandishi hao alisema
wamekuwa wakitoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo
juu ya mafuta na gesi.

Lupokela alisema waandishi wa habari ndiyo wanaohabarisha jamii
kupitia vyombo vyao na wananchi watatambua namna rasilimali ya mafuta
na gesi itakavyowanufaisha pindi wakielezewa kupitia magazeti, tv,
redia na mitandao.

“Hata zile vurugu za awali kwenye baadhi ya mikoa ya kusini ilitokana
na jamii kutoelewa ila baada ya wao kupatiwa elimu kuwa nao
watanufaika na rasilimali hizo hivi sasa hali imetulia na shughuli
zinaendelea ipasavyo,” alisema.

Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari wa mkoa wa Arusha (APC)
Claud Gwandu alisema suala la elimu ya mafuta na gesi ni muhimu
kutolewa kwa waandishi wa habari ili waweze kufikisha kwa jamii kwa
undani zaidi.

Gwandu alisema waandishi wa habari wangepaswa kupelekwa maeneo ya nje
ya nchi kupata mafunzo ikiwemo nchi ya Norway ambayo iligundua gesi
mwaka 1960 ili kuona wananchi wa eneo hilo walivyonufaika kupitia
nishati hiyo.

“Nakumbuka gesi asilia ya Songosongo iligundulika nchini mwaka 1974
ila baba wa Taifa akasema iachwe kwanza ili watanzania wapate elimu
kwa ajili ya kufahamu na kunufaika na rasilimali hiyo muhimu kwa nchi
yetu,” alisema.


No comments:

Post a Comment