Waandishi wa habari wa Mkoa wa
Manyara, wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya intaneti kwa uandishi wa
habari wa kisasa kwa ajili ya kutafuta habari, mawasiliano ya mtandao, kuchapisha
habari makazini mwao.
Kaimu mkurugenzi wa Taasisi ya vyombo
vya habari kusini mwa bara la Afrika, tawi la Tanzania, Andrew Marawiti,
akizungumza jana mjini Babati alisema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa
matumizi sahihi ya intaneti.
Marawiti alisema mafunzo hayo
yatawasaidia kutambua usalama wa teknolojia ya habari na umuhimu wake kwa
waandishi, matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, umuhimu wa kuzingatia
maadili ya uandishi wa habari kwa intaneti.
“Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Misa Tan
kwa kushirikiana na mfuko wa vyombo vya habari, mawasiliano na maendeleo
Finland Vikes Foundation kwa msaada wa Wizara ya mambo ya nje ya Finland,”
alisema Marawiti.
Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo
hayo Seif Jigge alisema hayo ni mafunzo ya tatu kuyatoa kwa waandishi wa
habari, kwani awali aliwaongezea uwezo wa habari za intaneti waandishi wa mikoa
ya Mtwara na Kilimanjaro.
Jigge alisema kupitia mafunzo haya
waandishi hao watakuwa na uwezo zaidi wa kupata taarifa zao kupitia vyanzo
husika na kutambua namna ya kuhifadhi kwa usalama kwenye mafaili yaliyopo katika
kompyuta ili zisivamiwe na virusi.
Mmoja kati ya mwandishi aliyeshiriki mafunzo
Restituta Fissoo alisema alijifunza kupata habari kwenye vyanzo vya uhakika
ikiwemo takwimu au habari za wizara kuliko kutafuta katika mitandao ya vyanzo
visivyo na uhakika.
Mwandishi mwingine Baraka Ole Maika,
alisema amejifunza mengi kupitia mafunzo hayo ikiwemo namna ya kuhifadhi taarifa
zake kwa usalama zaidi, kufahamu teknolojia ya habari kwa upana wake na kupata
anuani ya vyanzo vya habari.
No comments:
Post a Comment