Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
makazi, William Lukuvi amezindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kiteto
Mkoani Manyara, ambalo kwa kiasi kikubwa litamaliza migogoro ya ardhi iliyokuwa
inawakabili wananchi wa eneo hilo.
Awali, wananchi wa wilaya hiyo iliwabidi
wafuate huduma hiyo umbali wa kilometa 300 kwenda na kurudi wilayani Simanjiro
ambapo kuna baraza kama hilo, ili kufungua mashauri yao kwenye masuala ya ardhi
au nyumba.
Akizungumza wilayani Kiteto wakati
akizindua baraza hilo, Lukuvi alisema baraza la Kiteto na Lushoto ni miongoni
mwa mabaraza 47 yatakayozinduliwa hivi karibuni kwenye wilaya mbalimbali ambazo
hazina mabaraza.
Alisema baraza hilo litawasaidia
wananchi wa Kiteto kuondoa kero ya kufuata huduma hiyo wilayani Simanjiro kwani
kati ya kesi 150 zinazofanyika kwa mwaka wilayani Simanjiro, kesi 100
zinawahusu watu wa wilaya ya Kiteto.
“Lengo la serikali ya awamu ya tano ya
Rais John Magufuli ni kumaliza migogoro ya ardhi hivyo kupitia haya mabaraza ya
ardhi na nyumba na katika vijiji tutaweka matumizi bora ya ardhi ili kusiwepo
na migogoro,” alisema Waziri Lukuvi.
Alisema mpango wa matumizi bora ya ardhi
utasababisha wakulima na wafugaji kutogombana kwani kila kijiji kitatenga eneo
la mashamba, malisho ya mifugo, makazi, sehemu za ibada na huduma nyingine na
kuondokana na migogoro.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera
alisema baraza hilo litasaidia kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi
iliyokithiri kwani awali wananchi wengi walikuwa wanafika mjini Babati kutoa
malalamiko yao ya migogoro ya ardhi.
Hata hivyo, Dk Bendera aliwataka
Mwenyekiti wa baraza hilo la Kiteto Charles Mnzava na wazee wa baraza kutenda
haki kwa wananchi wa Kiteto wakati wa kuendesha mashauri hayo ili jamii ione
faida ya kuwepo kwa baraza hilo.
“Sasa wananchi waliokuwa wanakwenda
Simanjiro kuhudumiwa wamerahisishiwa kwa kuletewa baraza hapa Kiteto ila isiwe njia
ya kupokea rushwa na kuwa kero kwa jamii, tendeni haki ili watu waridhike,”
alisema.
Mbunge wa jimbo la Kiteto, Emmanuel
Papian alimshukuru Waziri Lukuvi kwa kuzindua baraza hilo kwani litasaidia kwa
namna moja au nyingine kumaliza migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa imekithiri
kwenye eneo hilo la Kiteto.
“Kupitia baraza la ardhi na nyumba hapa
Kiteto huu ndiyo utakuwa mwisho wa kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwani awali
tulikuwa tunateseka kwenda Simanjiro kwani jamii ilikuwa inatumia gharama
kubwa,” alisema Papian.
Alitoa ombi kwa Waziri Lukuvi kusaidia
upimaji wa viwanja vyote vya wilaya hiyo ili uwekwe kwenye mpango wa matumizi
bora ya ardhi, kwani huo utakuwa mwisho wa migogoro yote ya ardhi iliyokuwa
imekithiri Kiteto.
No comments:
Post a Comment