Wazee 500 wakiwemo vikongwe100 wa Mji mdogo wa Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamepatiwa msaada wa magunia 100 ya mahindi
yaliyotolewa na Mkurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne Hussein Gonga.
Mwenyekiti wa Saidia wana jamii Tanzania (Sawata) Mohamed
issa Mughanja akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya hiyo Mahmoud Kambona alisema
msaada huo umetolewa na Gonga kwa ajili ya wazee wa shirika la Mwasi.
Mughanja alisema zaidi ya kuwapatia msaada huo wa magunia 100
ya thamani ya sh7 milioni, Gonga pia amewafungulia bima ya afya ya jamii (CHF)
wazee hao ili wapate matibabu pindi wakiugua mara baada ya wazee hao kuomba
hayo.
“Aprili mwaka jana Sawata ilimwandikia barua Gonga ya
kukutana na wazee wa Mirerani na kuona namna ya kuwasaidia na mwezi Octoba
alikutana nao na aliwaahidi kuwapa chakula magunia 100 na kuwafungulia bima ya
afya” alisema.
Ofisa mwandamizi wa Sawata, Mohamed Shauri akisoma risala ya
kwa mkuu wa wilaya hiyo, alisema asasi yao ilianzishwa mwaka 2009 kwa kuisaidia
utekelezaji wa kilimo, visima na sera ikiwemo elimu, ushauri na kutafuta
wahisani.
Shauri alisema Sawata imeomba ardhi maeneo ya vijiji vya
Kilombero, Magadini na Ngage, ili kuwajengea uwezo wakulima wa kilimo hai cha
mboga mboga na matunda kwa njia ya umwagiliaji na kupatiwa mikopo ya pembejeo
siyo na riba.
“Hata hivyo, Sawata na makundi iliyonayo tunakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo vitendea kazi vya ofisi, wazee wetu wanachangamoto
nyingi na ukosefu wa ardhi ya kilimo kwani mpango wetu ni kutumia kilimo hai,”
alisema.
Kwa upande wake, mkuu wa wilaya hiyo Mahmoud Kambona
aliwataka wawekezaji wengine wa eneo hilo kuiga kitendo cha Gonga kwa
kuwasaidia watu wenye uhitaji ikiwemo wazee ambao wanahitaji msaada.
“Japokuwa madini ya Tanzanite yanapatikana kwenye wilaya yetu
ya Simanjiro lakini watu wanaofaidi ni kutoka nje ya eneo hilo, hivyo
wawekezaji wengine wanatakiwa kuiga mfano wa Gonga kwa kusaidia jamii,” alisema
Kambona.
No comments:
Post a Comment