Zaidi ya nyumba 25 za Kata ya Msitu wa Tembo na Mji mdogo wa
Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ikiwemo darasa la shule ya msingi Zaire
zimeezuliwa mapaa baada ya kutokea upepo mkali.
Kwenye kata ya Msitu wa Tembo kijiji cha Magadini nyumba 17
ziliezuliwa mapaa na kata ya Mirerani na Endiamtu zaidi ya nyumba nane
ziliezuliwa kutokana na upepo huo mkali uliotokea kwa nyakati
tofauti.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo, mkuu wa wilaya hiyo Mahmoud
Kambona alisema zaidi ya nyumba hizo kuharibika, hakuna mtu aliyejeruhiwa wala
kufariki dunia kutokana na tatizo hizo ila kaya kadhaa zimekosa makazi.
Kambona alisema baada ya tukio hilo alitembelea kwenye baadhi
ya maeneo yaliyokumbwa na tatizo hilo na ameshamuagiza mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri ya wilaya hiyo Lucas Mweri kukarabati darasa hilo lililoezuliwa
paa.
“Hata hivyo, nyumba nyingi zilizoezuliwa paa ni zile ambazo
zimejengwa kwa kutumia matofali ya udongo na nimeiasa jamii kujenga nyumba zao
kwa matofali ya udongo ili ziwe madhubuti kuepuka matatizo,” alisema Kambona.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kitongoji cha Twiga Anthony
Musiba alisema kwenye kitongoji chake ni zaidi ya nyumba tano zimepata dhoruba
ya kuezuliwa mapaa kutokana na upepo huo ila nyingine zimebomoka ukuta.
“Kwa tathimini ya haraka ni nyumba tano zimeezuliwa mapaa
ikiwemo ya mjane Farida Juma ambayo paa lake lilitolewa na upepo na kutupwa
kwenye nguzo ya umeme, pia vitongoji vingine vimeathirika” alisema Musiba.
Akizungumza baada ya ajali hiyo, mjane huyo Farida Juma
alisema hivi sasa wamehamia kwa mmoja kati ya majirani zao, ili kujisitiri
baada ya nyumba yao kuezuliwa na paa hivyo waangaliwe kwa jicho la huruma zaidi
kwa msaada.
“Tunaiomba serikali na wasamaria wema watusaidi kwani tuna
wakati mgumu hivi sasa ukizingiatia sisi ni wajane baada ya mtu tuliyekuwa
tunamtegemea mchimbaji madini marehemu Dotto Ruta na sasa hatuna mwingine,”
alisema.
No comments:
Post a Comment