Shule
ya sekondari Mgutwa ya Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imeazimia kugawa miti
1,500 kwa shule za msingi na sekondari za mji mdogo wa Mirerani ili kupambana
na majanga ya upepo na mmomonyoka wa ardhi.
Akizungumza na wageni waliotembelea shule hiyo, meneja wa shule hiyo Monica Mlemeta,
alisema wao ni wana mazingira, hivyo wataendelea kupanda miti mingi zaidi japo
eneo hilo waliloligeuza kuwa la kijani tofauti na awali.
Mlemeta
alisema shule hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne, ina lengo
la kuanzisha kidato cha tano hadi cha sita, ili kuboresha elimu ya eneo hilo la
Simanjiro pamoja na kuzidi kutunza mazingira kwa kupanda miti mingi.
Alisema
shule hiyo mwaka 2014 na 2015 iliotesha miti 1,000 ya kivuli na 300 ya matunda
ili kutunza mazingira hivyo wanataka na shule nyingine zioteshe miti kwa kasi
kubwa kwa ajili ya kuondokana na hali ya ukame na jangwa.
“Tutahakikisha
miti hiyo inagawiwa kwa uwiano sawa kwa kila shule ya sekondari na msingi
inayozunguka mji mdogo wa Mirerani na tutafuatilia ukuaji wake kwa ukaribu ili
kila mche umemea na siyo kufa,” alisema Mlemeta.
Mratibu
wa asasi ya Community Education resources foundation, Godfrey Lema walioipatia
shule ya Mgutwa miti hiyo 1,500 alisema lengo lao ni kuhakikisha wanatunza
mazingira na kuondokana na ukame uliopo katika eneo hilo.
Alisema kwa kushirikiana na asasi za Nick’s Eco
safaris na Moivaro jitegemee family wamefanikisha hilo, japo ardhi ya eneo hilo
ina mwamba na magadi, uongozi wa shule umelibadili kuwa la kijani, kwa
kuendeleza utunzaji mazingira na kuwa mfano wa kuigwa.
“Wageni
wetu Megan Allen kutoka Marekani na Juliane Friedrich wa Ujerumani, wamefurahia
ukijani uliopo hapa na tutahakikisha tunaendelea kuiunga mkono shule hii, kwani
imekuwa mfano bora wa utunzaji mazingira,” alisema Lema.
Alisema
elimu ya mazingira inatakiwa kutolewa kwa sehemu kubwa ya jamii ya wananchi wa
wilaya ya simanjiro, ili kuhakisha wanapanda miti kwa wingi kwani ndiyo vyanzo
vya mvua na kupata kivuli, matunda na hewa safi.
No comments:
Post a Comment