Rais
wa shirikisho la vyama vya madini nchini (Femata) John Bina amesema migogoro
mingi ya madini baina ya wachimbaji wadogo na wachimbaji wakubwa inasababishwa
na sheria mbovu za madini zinazotumika hivi sasa.
Bina
alidai kuwa sheria nyingi za madini ambazo ni mbovu zimenakiliwa kutoka nchini
Uingereza, ambapo hakuna madini ya vito ya Tanzanite na kutumika hapa nchini
hivyo kusababisha migogoro ya mara kwa mara ambayo haimaliziki.
Akizungumza kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite ya mji mdogo wa Mirerani Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara, alisema inatakiwa sheria hizo kandamizi ziondolewe
ili wachimbaji wadogo wafanye kazi zao bila kuonewa.
Alitaja
miongoni mwa sheria zinazowakandamiza wachimbaji wadogo kuwa ni sheria ya
kuchimba madini ya vito ya Tanzanite kwa njia ya wima ili hali jiolojia ya
madini hayo yanataka yachimbwe kwa njia ya mshazari.
Alisema
kutokana na madini hayo kuwa Tanzania pekee, ingetakiwa sheria, kanuni na taratibu
za uchimbaji wa madini ya Tanzanite uwe wa kipekee, kuliko hivi sasa
wanapochukua sheria za nje na kuendelea kuzitumia hapa nchini.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema)
Sadiki Mneney alisema japokuwa tume nyingi ziliundwa na serikali ili
kuhakikisha migogoro hiyo inamalizia lakini hazikufanikiwa.
“Tume
nyingi zimeundwa na kufika Mirerani ili kumaliza migogoro yetu na mchimbaji
mkubwa ila zikashindwa kumaliza ikiwemo ya Brigedia Jenerali Robert Mboma, Mang’enya,
Jaji Mark Bomani na wabunge 25,” alisema Mneney.