Saturday 7 February 2015

WASOMALI WAKAMATWA KITETO



Jeshi la polisi Mkoani Manyara limefanikiwa kuwakamata wasomali 31 kati ya 53, ambao ni wahamiaji haramu waliokuwa wanasafiri Wilayani Kiteto kuelekea mikoa jirani kwa lengo la kufika nchini Afrika kusini.

Hata hivyo, wasomali wengine 22 walifanikiwa kutorokea sehemu isiyojulikana wilayani humo, baada ya gari aina ya Fusso waliyokuwa wanasafiria kupata ajali na kuanguka japokuwa hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa au kufa ajalini hapo.

Akithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP) Christopher Fuime alisema wasomali hao walikamatwa Januari 6 mwaka huu saa 7 mchana wilayani Kiteto.

Kamanda Fuime alisema wasomali hao walikamatwa kwenye kitongoji cha Twanga Namelock, katika kata ya Partimbo na walikuwa wanaelekea nchini Afrika kusini kupitia mikoa ya Dodoma, Iringa na Mbeya.

Alisema kuwa wasomali hao 53 walikuwa wamepakizwa kwenye gari aina ya Fusso lenye namba za usajili T 227 BBV, lililokuwa likiendeshwa na Nuru Ibran (35) mkazi wa mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro.

“Wasomali hao walipofika kwenye kitongoji hicho wakiwa kwenye gari walipata ajali na baadhi ya watu walitoa taarifa polisi na sisi tukafanikiwa kufika mara moja na kuwakamata wahamiaji hao haramu,” alisema Kamanda Fuime.

Hata hivyo, kamanda Fuime alisema bado wanaendelea na jitihada za kuwatafuta wasomali hao wengine 22 ambao walitoroka baada ya kutokea kwa ajali hiyo na aliwaomba wananchi watoe ushirikiano ili kutekeleza jambo hilo.

Naye, mkazi wa mjini Kibaya wilayani humo, Mbwana Jumaa alipongeza jitihada za polisi kufanikisha kukamatwa kwa wasomali hao, kwani taarifa ya kuonekana kwa wasomali hao walipozipata walifika kwenye eneo la tukio kwa muda mfupi.  

“Hapa kuna mchezo fulani mchafu unaofanywa na baadhi ya watu, hivyo polisi ichukuwe hatua kwani hao wasomali ni wageni na hawawezi kujua mazingira ya huku ni lazima wakamatwe,” alisema John Mollel mkazi wa kijiji cha Partimbo.

No comments:

Post a Comment