Shule ya msingi Endiamtu ya
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, yenye upungufu wa matundu 19 ya choo,
imepatiwa msaada wa mifuko 34 ya saruji iliyotolewa na kwaya ya Mirerani
Central ya Kanisa la Wasabato SDA.
Katibu wa Kanisa hilo, Benson
Nyaura akizungumza jana wakati akikabidhi mifuko hiyo 34 ya saruji kwa Diwani
wa kata ya Endiamtu Lucas Zacharia alisema kanisa ni taasisi inayojali mahitaji
ya jamii hivyo wamejitoa ili kusaidia wanafunzi hao.
Nyaura alisema kila wakati Kanisa
hilo linashirikiana na wananchi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazowakabili ili kuhakikisha kwa namna moja au nyingine wanatatua matatizo
yanayoizunguka jamii.
Kwa upande wake, Diwani wa kata
ya Endiamtu Lucas Zacharia aliwapongeza wana kwaya hao kwa kujitolea kiasi
hicho cha saruji, ambapo ikichanganywa na fedha zilizotengwa, zitawezesha
kujengwa kwa choo kingine cha shule hiyo.
Zacharia alisema alipochaguliwa
kuwa Diwani mwaka 2010 alikuta shule hiyo ina majengo ya madarasa mawili na
wanafunzi wa kuanzia darasa la kwanza hadi la sita, ila sasa wameongeza
madarasa mengine manne na ofisi ya walimu.
“Mimi kwa kushirikiana na jamii
na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, tumeweza kuiendeleza shule hii ambayo
mwaka jana ifanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba hivyo kuonga
kitaaluma,” alisema Zacharia.
Naye, Ofisa mtendaji wa kata ya
Endiamtu Edmund Tibiita alipongeza jitihada za Diwani huyo kuipa kipaumbele
shule hiyo ya msingi ambayo awali ilikuwa inadharaulika kuwa ipo porini na sasa
imepiga hatua kubwa hasa kitaaluma.
“Sasa hivi shule hii ina vyumba
sita vya madarasa, kutoka vyumba viwili vilivyokuwepo mwaka 2010 na Diwani
Lucas amechangia fedha zake binafsi sh5 milioni kwa ajili ya kuendeleza shule
hii na anafaa kupongezwa,” alisema Tibiita.
No comments:
Post a Comment