AMUUA MKEWE KWA WIVU WA MAPENZI
Ikiwa leo ni siku ya wapendanao mkazi wa Kijiji cha Dirimu Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, amemuua mkewe kwa kumchinga shingo kama kuku na yeye kujiua kwa kujinyonga kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Mwanaume huyo ambaye amezaa watoto nane na mke wake, inadaiwa kuwa walikuwa wanaishi nyumba moja ila baba alikuwa akitoka nyumbani asubuhi anarudi usiku na hajui familia yake imeshindaje wala imekula au haijala chakula.
Akizungumza na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, SSP Christopher Fuime alisema vifo hivyo vilitokea Februari 12 saa 10 jioni kwenye pori la kijiji cha Dirimu katika wilaya ya Mbulu.
Kamanda Fuime aliwataja marehemu hao kuwa ni Qambadu Kwatlema (45) mkulima na mkazi wa kijiji hicho ambaye alimuua mke wake Amsi Matle (43) kwa kumchinja na kisu shingoni na kumkatakata sehemu nyingine za mwili.
“Chanzo cha vifo ni wivu wa kimapenzi kwani mwanaume alihisi mke anatoka nje ya ndoa yao na inasemekana siku moja kabla ya kifo chake Kwatlema alisema atamuua hawara yake au kumuua mkewe,” alisema Kamanda Fuime.
Alisema baada ya Kwatlema kumuua mkewe naye alikimbilia porini jirani kidogo na wanapoishi na kujinyonga na miili ya marehemu hao imeshazikwa kwenye eneo moja baada ya uchunguzi wa miili hiyo kufanywa na daktari na polisi.
Hata hivyo, mmoja kati ya shuhuda wa tukio hilo Daudi Yuda alidai kuwa jana yake kabla ya tukio hilo, Kwatlema alikuwa anamlalamikia jirani yake ana mahusiana na mkewe hivyo atafanya jambo ambalo litaacha historia kwao.
“Sisi tulidhani ni utani anaongea wakati akinywa pombe na kulewa kumbe mwenzetu alikuwa na wivu kweli ila hakuweza kumuua mtu aliyekuwa anahisi anatembea na mke wake akaishia kumuua mkewe,” alisema Yuda.
Naye, Scolastika Sulle alisema wakazi wa eneo hilo wamesikitishwa na vifo hivyo vya kikatili, kwani Kwatlema alimuua kwa kumchinga kama kuku na kumtoa utumbo nje baada ya kumkata na kumuachia shimo mgongoni.
“Watoto nane wameachwa yatima bila wazazi lakini pia mtoto mdogo wa mwisho mwenye umri wa miaka mitatu ndiye anayewasikitisha wananchi wa kijiji hiki kwani wameachiwa majonzi makubwa sana,” alisema Sulle.
No comments:
Post a Comment