Tuesday, 8 May 2012

WAFUGAJI NA WAKULIMA WALILIA ARDHI KWENYE KATIBA

Na Joseph Lyimo
WAKAZI wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara wamedai kuwa Katiba ya sasa
inawabana wananchi wa vijijini juu ya umilikishwaji ardhi hivyo katiba
mpya inatakiwa kutoa kipaumbele  cha umilikishwaji ardhi kwa wakulima
na wafugaji.

Hayo yamesemwa juzi na wakazi wa wilaya hiyo kwenye kongamano la
mchakato wa Katiba mpya lililoandaliwa na Mtandao wa Asasi za kiraia
wilayani Kiteto (KCS Forum) na kufadhiliwa na The Foundation For Civil
Society.

Mratibu wa asasi ya Naadutaro,Lembulung Ole Kosyando alisema katiba
iliyopo hivi sasa ina upungufu mkubwa wa suala la umilikishwaji ardhi
kwa jamii japokuwa katiba hiyo imeeleza kwamba ardhi ni mali ya umma.

Kosyando alisema sheria ya ardhi namba nne inazungumzia juu ya ardhi
ya miji na sheria namba tano ya ardhi inazungumza vijiji lakini sheria
hiyo namba nne kila wakati imekuwa kikwazo kwa kuimeza sheria namba
tano.

“Wananchi wa vijijini,wakulima na wafugaji hawana uhakika na matumizi
ya ardhi yao kwani kila mara sheria namba nne ya ardhi ya miji
inakinzana nao na kuwafanya wafukuzwe au kuhamishwa kwenye ardhi yao,”
alisema Kosyando.

Naye,Katibu wa UVCCM wilaya ya Tanga mjini,Gerald Augustino alisema
watanzanita wanatakiwa kujengewa uwezo kuhusu suala la ardhi kwani
rasilimali hiyo ndiyo urithi pekee wa maisha yao

“Katiba mpya inatakiwa kulinda kipengele cha ardhi kwa wananchi ambayo
ndiyo utajiri wao kwani bila kutoa kipaumbele kwenye ardhi hawatakuwa
na uhakika wa maisha yao,” alisema Augustino.

Naye,Mratibu wa KCS Forum,Nemence Iriya alisema lengo la kuandaa
kongamano hilo ni kuwaweka tayari wakazi wa wilaya hiyo ili Tume ya
kukusanya maoni ya katiba mpya itakapofika wapate cha kuzungumza.

“Kupitia kongamano hili mtakuwa tayari kutoa maoni yenu na mtatambua
nini cha kuzungumza mara baada tume ya katiba mpya itakapowafikia na
elimu mliyoipata hapa mkaieneze kwa wenzenu ambao hawakufika,” alisema
Iriya.

Pia,aliwataka wakazi hao watambue kuwa maoni ya Katiba mpya
yaliyotolewa kwenye kongamano hilo yatapelekwa kwenye tume hiyo
kupitia mjumbe wao Humphrey Polepole ambaye anaziwakilisha asasi
zisizo za kiserikali.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment