VIJANA WAHAMISHA TAWI LA CHAMA
Na Joseph Lyimo
KATIKA tukio ambalo halikutarajiwa vijana zaidi ya 50 waliokuwa
wanachama wa CCM Tawi la Cairo Mji mdogo wa Mirerani Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara wameishusha bendera ya Tawi hilo na
kuipandisha ya Chadema.
Tukio hilo lilitokea juzi,baada ya wakereketwa hao kushusha bendera
hiyo na ghafla wakajiunga kwenye ufurukutwa kwa kudai kuwa CCM
imepoteza dira na mwelekeo hadi kusababisha maisha kuzidi kuwa magumu
na mfumuko wa bei.
Wakizungumza na waandishi wa habari,vijana hao walidai kuwa baadhi ya
viongozi wa CCM wa Tawi hilo wanaendesha shughuli za chama hicho
kibabe hivyo wameamua kuwaachia chama chao na kujiunga na chama cha
wajanja.
Walisema pia wamehamaka baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM mkoani
Arusha James Ole Millya kuhamia Chadema hivyo na wao wanafuata nyayo
zake kwani chama hicho ni chama makini chenye kujali watu wanyonge.
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walishangazwa na kitendo hicho
kwani walidai kuwa hawajawahi kuona bendera ya chama ya Tawi
ikishushwa na kuwekwa ya chama kingine zaidi ya bendera za kwenye
mashina na siyo Tawi.
Hata hivyo,Mwenyekiti wa CCM Tawi la Cairo,Sifael Saitore aliwataka
wanachama wa eneo hilo kutokata tamaa na kutetereka kutokana na
kitendo hicho kwani huo ni upepo tu na utapita na kutulia kama
ilivyokuwa awali.
“Hata hivyo sisi hatuna jengo la ofisa ila tuna kiwanja ambacho
tunategemea kujenga ofisi na hapo mahali ofisi yetu ilipokuwa kabla
Chadema hawajaweka tawi lao ni eneo la chini ya mti wa Cairo bar na
siyo ofisi,” alisema Saitore.
Alisema hawezi kuzuia utashi na mtazamo wa vijana hao kuweka bendera
ya Chadema kwani kila mtu ana uhuru wa kufanya jambo analolitaka na
hawezi kulazimisha mtu ale wali wakati anataka kula ugali.
Alisema hivi sasa wana mikakati ya kutafuta eneo lingine kwa ajili ya
kuweka ofisi yao kwani eneo la awali lilikuwa siyo mali ya chama ni
mali ya mtu binafsi hivyo wanatafuta eneo lingine kabla ya kujenga
ofisi yao ya kudumu.
MWISHO.
VIONGOZI MJI WA MIRERANI WAPANDA MITI 200
Na Joseph Lyimo
ILI kuunga mkono jitihada za Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal za
uhifadhi wa mazingira nchini,viongozi wa mji mdogo wa Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wamepanda miti 200 ya kustawisha mji
huo.
Akiongoza zoezi hilo la upandaji wa miti juzi,Mwenyekiti wa Mamlaka ya
mji huo,Albert Siloli amesema miti hiyo imepandwa kwenye maeneo
tofauti ikiwemo taasisi mbalimbali za Serikali.
Siloli aliongoza upandaji miti akiwa na Makamu Mwenyekiti wake,Hussein
Msokoto,Mwenyekiti wa Kairo,Wilbert Nyari,Mwenyekiti wa Kilimahewa
Joseph Masasi,Ofisa Mtendaji wa mji huo,Nelson Msangi na Ofisa
Mtendaji wa kata ya Endiamtu Edumund Tibiita.
Alisema walipanda miti 30 shule ya msingi Tanzanite,miti 20 shule ya
sekondari Mirerani Benjamin Mkapa,miti 20 shule ya msingi
Endiamtu,miti 50 kituo cha afya,miti 30 ofisi ya Tarafa,na miti 20
sokoni na miti 30 kwenye nyumba za watumishi.
“Hivi karibuni tulikaa kikao cha Baraza la Mamlaka ya mji mdogo na
kuazimia kila kaya ipande miti isiyopungua 10 na kamati za vitongoji
zitasimamia zoezi hilo ili kuhakikisha mazingira ya mji yanakuwa
mazuri,” alisema Siloli.
Alisema nia na madhumuni ya zoezi hilo ni kuhakikisha kauli mbiu ya
kuufanya mji mdogo wa Mirerani unakuwa wa kijani unafanikiwa na lengo
hilo linatimizwa kutokana na mwitikio wa jamii na viongozi wao.
“Pia kwenye kikao hicho tuliazimia kuwa kila taasisi ya Serikali
iliyopo mji mdogo wa Mirerani ihakikishe kuwa inapanda miti 30 kwa
ajili ya kuunga mkono zoezi hili la kuufanya mji wetu una kuwa wa
kijani,” alisema Siloli.
No comments:
Post a Comment