Joseph Lyimo,Simanjiro
WAKAZI wa kijiji cha Kimotorok Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara wamelalamikia kitendo cha walinzi wa hifadhi ya
Mkungunero kufanya ujangili wa kuwinda wanyamapori kijijini hapo na
kuuza wilayani Kondoa.
Wakizungumza na waandishi wa habari juzi,wakazi hao wamedai kuwa
walinzi hao wameanzisha mtindo huo na kisha kuwasingizia wakazi wa
kijiji hicho kwamba ndiyo wanaohusika na kuwinda wanyamapori kwenye
hifadhi hiyo.
Akithibitisha kutokea kwa vitendo hivyo Diwani wa kata ya
Loiborsiret,Lucas Ole Mukus alisema walinzi hao wamekuwa wakiwinda
wanyamapori na kuuza kisha huwasingizia baadhi ya wakazi wa kijiji
hicho kuwa ndiyo wamehusika.
Ole Mukus ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara alisema hivi
karibuni gari la hifadhi hiyo aina ya Land Rover TDI lenye namba za
usajili STK 3629 lilikutwa na ngozi na nyama ya pundamilia wawili
waliowinda kwa wizi.
“Mhifadhi wa wilaya ya Simanjiro Saigurani Mollel alifuata nyayo za
gari hilo na kubaini likiwa na nyara hizo za Serikali na hadi hivi
sasa zimehifadhiwa kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho Melau Kunyae,”
alisema Ole Mukus.
Aliongeza kuwa walinzi wa hifadhi hiyo pia waliwakamata watoto wawili
waliokuwa wanachunga mifugo yao na kuwasingizia kuwa walikuwa
wanawinda na kutaka kuwapeleka mjini Babati kwa ajili ya kuwashtaki
mahakamani.
“Nitahakikisha suala hili nalifuatilia kwa nguvu zote kwani walinzi
hao ndiyo wangepaswa kusimamia ulinzi hifadhini hapo lakini wanafanya
uhalifu kwa kuwinda na kuwasingizia wananchi wangu,” alisema Ole
Mukus.
Hata hivyo,mmoja kati ya kiongozi wa hifadhi ya Mkungunero ambaye
hakupenda kutaja jina lake kwa vile siyo msemaji alisema matukio
yanayofanywa na watumishi wa hifadhi hiyo walishayasikia.
Alisema watumishi wote wanaotuhumiwa wameshapata majina yao na hivi
sasa uongozi wao unayafanyia kazi kabla ya kuwachukulia hatua kali
walinzi wote na madereva ambao wanahusika na matukio hayo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment