Wednesday, 21 June 2017

OLE SENDEKA AMTUMIA SALAMU LOWASSA



Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amemtuma mbunge wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya kumpelekea salamu aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa kwa kumuunga mkono Rais John Magufuli, kwenye kulinda rasilimali za Taifa. 

Akizungumza kwenye mazishi ya marehemu mama yake Raheli Sendeka yaliyofanyika kwenye Kijiji cha Losokonoi Wilayani Simanjiro, Ole Sendeka alimtuma Ole Millya afikishe salamu zake za shukrani kwa Waziri Mkuu mstaafu Lowassa.

Alisema ni jambo zuri kwa Lowassa kuunga mkono jitihada za dhati za Rais Magufuli kulinda rasilimali za nchi na baada ya kusoma magazeti kuwa Lowassa amempongeza Rais Magufuli naye hana budi kumpongeza Lowassa kwa hilo. 

"Nanyi wabunge mkiwa bungeni muungeni mkono Rais wetu Magufuli anavyotetea rasilimali za nchi ili madini yanayochimbwa yaweze kuwanufaisha watanzania waweze kupata huduma zao za msingi kupitia madini yao, " alisema Ole Sendeka.

Pia, aliwapongeza wabunge waliohudhuria mazishi hayo, akiwemo Mwenyekiti wa kamati ya miundombinu Norman Sigala, mbunge wa jimbo la Babati Vijijini, Vrajlal Jituson na Ole Millya, akiwataka waendeleze umoja kwa kutetea maslahi ya jamii wakiwa Bungeni. 




Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kaskazini kati, Dk Solomon Masangwa alisema watanzania wanapaswa kuuenzi upendo walioachiwa na Mungu.  

Dk Masangwa aliyasema japokuwa kuna msemo usemwao amani haipatikani ila kwa ncha ya uwanja, watanzania wasikubali hilo kwa kudumisha umoja uliopo ili kuendeleza amani iliyopo. 

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha, akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali alisema jamii inapaswa kumuenzi marehemu Raheli Sendeka kwa kuiga yale yote mema aliyokuwa anayafanya kipindi cha uhai wake. 

"Mmoja kati ya wajukuu wake Nailejileji Sendeka alisema bibi yake alimuasa kuwapenda watu wote ambao Mungu amewaweka kwenye maisha kwa kuwathamini wenye uwezo na wanyonge hivyo sisi sote tumuenzi kwa kuyatenda hayo," alisema Ole Nasha. 

Mbunge wa jimbo la Simanjiro, James Ole Millya alisema wakati aliposhinda ubunge wa jimbo hilo aliahidi kuwapenda na kuwapa ushirikiano wananchi wote wa wilaya hiyo bila ubaguzi wowote ule. 

"Mheshimiwa mkuu wa Mkoa wa Njombe, niliahidi kutobagua watu kwenye uongozi wangu na hivi ndivyo ninavyofanya ili kuweka pamoja jamii yetu ya jimbo la Simanjiro," alisema Ole Millya. 

Mmoja kati ya watoto wa marehemu huyo, Sumleck Ole Sendeka akisoma historia yake alisema mama yao Raheli alizaliwa mwaka 1927 eneo la Oleng'iding'idata, kijiji cha Lendanai wilayani Simanjiro. 

Alisema Raheli aliolewa na baba yao akiwa mke wa kwanza kati ya wake nane wa marehemu baba yao mzee Olonyokie Ole Sendeka na alijaliwa watoto 12, kati yao saba wako hai na watano walishafikisha, ameacha wajukuu 137,vitukuu 93 na kilembwe mmoja.

Alisema marehemu alibatizwa mwaka 1971 KKKT mtaa wa Orkesumet usharika wa Naberera na hadi anafariki alikuwa mshiriki mzuri wa maendeleo ya kanisa lake.

Alisema marehemu alianza kusumbuliwa na tatizo la kisukari mwaka 2000 na kupatiwa matibabu hospitali za KCMC, Mount Meru, Siima, St Thomas, Calvary Mirerani, Losokonoi na Lendanai hadi alipoaga dunia saa 6 usiku, Juni 9 mwaka huu.

Mwenyekiti wa kamati ya mazishi hayo mfanyabiashara Mathias Manga aliwashurukuru watu wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kwa ajili ya kufanikisha shughuli zote za mazishi hadi maziko.  

HIFADHI YA KITULO


Thursday, 15 June 2017

WATANZANIA WATAKIWA KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI KWENYE VITA YA KULINDA RASILIMALI



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga amesema watanzania wanapaswa kumuunga mkono Rais John Magufuli kwenye vita ya kulinda rasilimali za nchi aliyoianzisha.

Kamoga aliyasema hayo juzi kwenye maadhimisho ya siku ya albino
duniani, ambayo  kimkoa ilifanyika kituo cha 4 Angle mji mdogo wa
Haydom na alimwakilisha mkuu wa mkoa huo Dk Joel Bendera.

Alisema vita ya kulinda rasilimali ya nchi inapaswa kuungwa mkono
kwani utajiri wa nchi ya Tanzania haulingani na hali halisi iliyopo
kutokana na watu wachache kupora utajiri kupitia madini mbalimbali.






Alisema ana imani Rais Magufuli na watanzania kwa ujumla watashinda vita ya kulinda rasilimali kwani kupitia ripoti ya pili ya makania imeonyesha namna wananchi wanyonge wanavyoibiwa.

“Pamoja na kuathimisha siku ya albino duniani tunapaswa kumuunga mkono Rais Magufuli katika vita hii ya kusimamia na kulinda rasilimali za nchi kupitia madini yetu kwani nia ya dhati ameionyesha,” alisema Kamoga.



 

Mwenyekiti wa chama cha maalbino mkoani Manyara, Joseph Masasi alisema wanakabiliwa na changamoto ya kutobaini idadi kamili ya watu wenye ualbino mkoani humo hivyo kukosa takwimu sahihi.

Masasi alisema tatizo hilo linasababisha hata kukitokea tatizo lolote
linalohitaji msaada kwao inakuwa vigumu kwani wengine wanakosa
kutokana na kutobainishwa kwa idadi yao katika wilaya za mkoa huo.

Alisema pia wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa mafuta maalum ya
kujipaka kwa watu wenye ualbino yanayowasaidia kila siku ili
wasiathiriwe na mionzi ya jua na kusababisha baadhi yao kuathirika.

“Pamoja na hayo tunashukuru kwenye mkoa wa Manyara hakuna matukio ya watu wenye ualbino kuuawa au kukatwa viungo na watu makatili ila kuna badhi ya matishio madogo madogo,” alisema Masasi.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Joseph Mandoo alisema halmashauri yao itaendelea kushirikiana na uongozi wa ualbino kwa ajili ya kuhakikisha wanatoa msaada unaohitajika kwa watu hao.

Mandoo alitoa wito kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye ualbino kutowafisha ndani na badala yake wawafikishe kwenye sehemu husika ili pindi misaada itakapotolewa waweze kupatiwa.