Thursday, 12 January 2017

MAPADRI WA MANG'OLA

Mapadri wa Mang'ola walivyoisaidia jamii kiroho na kimwili

Na Joseph Lyimo

Kwa asili yake Tanzania ni nchi iliyobarikiwa sana na Mungu. Ni nchi yenye rasilimali nyingi inayokaliwa na wananchi wanaounganishwa na utaifa wao na kwa hiyo kuendelea kuwa nchi yenye amani ya kudumu na hivyo kuwa nchi yenye kuaminiwa na kutumainiwa.

Wananchi wanaipenda nchi yao na majirani na nchi rafiki wanaipenda Tanzania. Tatizo ni kwamba yewezekana wengi wetu hatuujui ukweli huo na ikiwa
tunaijua, basi tunadeka na ama hatutambui uhalisia kwamba unapopendwa na wewe upendeke. Ukipendwa leo nawe ukakataa kupendwa, kesho ukipenda wewe, utakataliwa na hutapendwa.Kupendwa ni bahati na siyo haki ya kudaiwa popote!

Nchi yetu inazo nchi rafiki ambao zina urafiki wa kinafiki lakini pia inazo nchi rafiki ambazo ni marafiki wa kweli na wanaoitakia nchi yetu mema kupitia wananchi wao wanaokuja kutembelea nchi yetu, kuwaona watu na mifumo yao ya kijamii, maisha yao na changamoto zao.

Wapo pia wanaokuja kuona rasilimali na fursa za uwekezaji. Pia, wapo watu binafsi kutoka nchi hizo rafiki, ambao huguswa na changamoto za watu wetu nao huingiwa na ukarimu wa kutaka kutusaidia kuondokana na changamoto hizo.

Tanzania imebahatika kupendwa kwa dhati kwa takriban miaka 40 sasa yaani tangia Mwaka 1976 na mapadri wawili Jose Aguilar Torner na Miguel Angel Lozano ambao ni wa Shirika la Roho Mtakatifu kutoka nchini Hispania.

Mwananchi wa Kijiji cha Narakauwo Kata ya Loiborsoit Tarafa ya Emboreet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Ole Mukusi ambaye aliwahi kuwa diwani wa kata hiyo na hivi sasa ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo anasema kwa mara ya kwanza mapadri hao kufika kwao Tanzania walipewa kituo cha kazi Parokia ya Emboreet, katika mbuga za Tukutta.

Ole Mukusi anasema mapadri hao wawili walifanya kazi kubwa parokiani hapo kwa kujenga majengo ya kuishi mapadri na masista, majengo ya kutolea huduma ya uhakika ya afya, zahanati yenye kutoa huduma ya wagonjwa wa nje OPD na pia kulaza wagonjwa, vitanda 30, huduma ya afya ya mkoba, huduma ya afya ya uokoaji kwa njia ya ndege (Flying Doctors Service) na kuimarisha huduma ya maji kutokea kwenye chanzo hadi katika shule ya Msingi na kupanua mtandao hadi kituo cha Afya.

 Anasema mapadri hawa walifanya kazi Emboreet Simanjiro hadi mwaka 1983 ambapo Padri Jose Aguilar Torner (maarufu kwa jina la Pepe) alipohamia Engikaret-Monduli na PadrI Miguel Angel Lozano (Maarufu kwa jina la Oloronyo) akahamia Loliondo-Ngorongoro mnamo mwaka 1985.

Anaeleza kuwa huko Engikaret, padri Pepe alijenga nyumba za kuishi mapadri na masista, kuboresha shule ya makatekista kuwa sekondari kwa majengo na vifaa vya kufundishia, kujenga kanisa na zahanati ambako huduma bora na ya uhakika ya afya ilitolewa kwa mara ya kwanza.

“Wakati wote huo, dawa nyingi na vifaa vya kisasa vililetwa kutoka Hispania na mara kwa mara wataalamu wabobezi wa maradhi mbalimbali walifika kutoa huduma za rufaa kwa wagonjwa wa maeneo walikofanya kazi mapadri hao na kwa njia hii, maisha ya wagonjwa wengi yaliweza kuokolewa,” anasema.

Anaongeza kuwa mwaka 1993, mapadri hawa walikutanishwa tena ili kufanya kazi pamoja, baada ya askofu wa Jimbo la Arusha, kuwatuma kwenda eneo la Mang’ola Chini ili kuchochea maendeleo ya kiroho na kimwili jambo ambalo wamelifanya kwa takriban miaka 23 kwa ufanisi mkubwa mno.

Anasema mapadri hao wawili Pepe na Miguel ni wabunifu mno na viongozi wenye moyo mkuu katika kuwahudumia watu wao bila kujali imani ya jamii ya maeneo ambako wanatoa huduma ya kiroho.

Huduma za kitaalamu za afya na mambo mengine.

Mapadre wa Mang’ola-chini, Pepe na Miguel ni watu ambao daima hufikiria njia za kupambana na matatizo yanayowakabili watu wao, katika kufanya hivyo, hukabiliwa na changamoto za ubabe na ukorofi wa baadhi ya viongozi na wanasiasa wenye mwelekeo usiokuwa na manufaa kwa jamii ya Mang’ola na Tanzania kwa ujumla wake, jambo ambalo huwawia vigumu mapadri hawa kukubaliana nalo.

Ole Mukusi anasema katika kuboresha utoaji wa huduma za kiafya, mapadri hawa wamejenga mahusiano na mashirika yenye kutoa huduma kwa mfano wataalamu wa meno, mifupa na masikio kutoka nchi ya Hispania.

Anasema wataalamu hawa huja kwa makundi yenye kutofautiana kwa ukubwa na kipindi cha kuja Mang’ola na idadi ya wataalamu katika makundi haya ni kuanzia watu nane hadi 16 na kwamba wanayapokea makundi matatu hadi manne kwa mwaka.

“Licha ya kuwa CBO ya WAVIU inalo Trekta, ambalo hulitumia kukodishia wakulima ili kupata fedha, mapadre huwapatia WAVIU huduma ya afya bure pamoja na chakula, mapadre hao wameanzisha CBO kwa ajili ya jamii ya Wahadzabe katika kuwasaidia waweze kupata mahitaji ya muhimu ya kibinadamu, kupitia utalii unaofanywa katika maeneo yao,” anasema.

Anasema kuwa mapadri hao wamewezesha uanzishaji wa shule mbili za awali kwa nia ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuwapatia watoto wa wananchi wa Mang’ola elimu.

Anasema kwa nyakati ambazo wataalamu wa huduma za rufaa kutoka Ulaya hawapo, kila inapolazimu mgonjwa anahitaji huduma ya dharura, gari la wagonjwa humsafirisha mhusika kwenye huduma Arusha au KCMC Mkoani Kilimanjaro na mara zingine Dar es salaam.

Anasema mapadri hao wamejenga mahusiano na shirika la La Arruzafa Foundation yenye makao yake Cordoba Hispania ambayo hufanya huduma mbalimbali za macho, ambapo wataalamu kutoka taasisi hiyo walifika Mang’ola mwaka jana na kwa wiki moja walihudumia wagonjwa wa macho 736 kati yao wagonjwa 600 walipewa miwani ya thamani kati ya sh65,000 na sh90,000 ya kuonea, kusomea na ya kukinga mionzi mikali ya jua.

Anasema upasuaji mkubwa ulifanyika mara 74 na zote zilifanyika vizuri na kwa muda wote huo, La Arruzafa Foundation iliwalipa watumishi wa kituo cha afya Mang’ola, posho zao za siku na zile za ufanyaji kazi wa ziada na kuwapatia huduma za chakula na malazi wagonjwa wasio na uwezo wa kujikimu au kujihudumia malazi na chakula.

“Upasuaji huo ulifanyika katika chumba cha upasuaji iliyosheheni vifaa vingi vya kisasa ambavyo wataalamu hao hupenda kushirikiana na wataalamu wetu wa wilaya na mkoa ili kuwajengea uzoefu katika matumizi ya vifaa hivyo,” anasema na kuongeza;

“Hata hivyo, kuna hofu kuwa wanafunzi wengi wa Mang’ola wanakabiliwa na uoni hafifu nyakati za giza kutokana na hali ya kijiografia na hivyo kuwa sababu ya wanafunzi wengi kupatiwa miwani ya kupunguza ukali wa mionzi mikali ya jua.”

Anasema mapadri wamewezesha uanzishaji wa shule mbili za awali kwa nia ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuwapatia wananchi elimu na kwa nyakati ambazo wataalamu wa huduma za rufaa kutoka Ulaya hawapo, kila inapolazimu
kwamba mgonjwa anahitaji huduma ya dharura, gari la wagonjwa humsafirisha mhusika kwenye huduma Arusha au KCMC mkoani Kilimanjaro na mara zingine Dar es salaam.

Jamii ya Mang’ola yawazungumzia mapadri hao

Mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo Antony John anasema japokuwa suala la kufanikisha maendeleo ya jamii ikiwemo shule, maji, miundombinu, afya ni jukumu la serikali, lakini viongozi hao wa dini wamejitahidi kwa uwezo wao kufanikisha hayo.

“Kutokana na hali hiyo viongozi hawa wa kiimani wanapaswa kukumbatiwa na kuungwa mkono kwani kwa muda wote waliokuwa hapa Mang’ola wametuonyesha kuwa wao ni watu wa maendeleo na wamebadili eneo hili likawa na maendeleo ya kutosha,” anasema John.

Hamisi Bakari mkulima wa vitunguu anasema mapadri hao wamekuwa wanatoa msaada kwa jamii ya eneo hilo bila kubagua dini au madhehebu hivyo serikali inapaswa kuwapa ushirikiano wa kutosha kupitia maendeleo wanayofanya katika eneo hilo la Mang’ola.

“Japokuwa wenyewe ni mapadri wa kanisa katoliki lakini wamefanikisha ujenzi wa msikiti kwenye eneo letu la Mangola hivyo kuunganisha mioyo ya watu wa madhehebu mengine na kitendo hicho kimetufanya tuwe ndugu moja japokuwa sisi ni watu wa imani tofauti,” anasema Bakari.

Rai kwa Rais John Magufuli

Ole Mukusi anasema pamoja na ukweli kuwa mapadri hawa wa Shirika la Roho Mtakatifu wamekuwepo nchini kwa takriban miaka 40 yaani kipindi muhimu cha maisha yao, hadi sasa bado wanakabiliwa na changamoto ya kupatiwa vibali vya kuishi hapa nchini ili kuwahudumia Watanzania bila wao kupata faida
yoyote binafsi.

“Kwa miaka yote waliyowatumikia watu wetu, bado wanaendelea kama vile ndio wanakuja leo nchini na kwa hiyo wanapatiwa kwanza visa ya kitalii ili hali mapadre hawa wanaisaidia serikali yetu katika kutekeleza jukumu la kuihudumia jamii yetu kiroho, kielimu na kiafya,” anasema.

Anaeleza kuwa mapadri hawa hupata usumbufu mkubwa kila wanapoomba vibali vya wataalamu wa afya kuingia nchini ili kutoa huduma ya bure kwa Watanzania.

“Pia wao huchukua muda mwingi kuvipata vibali hivi ambavyo hulipiwa fedha nyingi bila hata kujali kwamba wataalamu hawa wanakuja kuokoa bure maisha ya jamii ya Tanzania,” anasema Ole Mukusi.

Anasema Mungu anatutumikia kupitia wataalamu hawa na ndiyo sababu
wanaihudumia Tanzania kwa upendeleo mkubwa kwani wamefanya kazi nchini Benin miaka miwili, Equatoria Guinea miaka mitano, Madagascar miaka saba na Tanzania miaka 11 na bado wana nia na moyo wa kuendendelea kutoa huduma.

“Hapa kwetu, wanawapatia jamii huduma zao bure kwa kutumia vifaa walivyotoa kama msaada pamoja na kwamba vipo vingine ambavyo wanakuja navyo na kurudi navyo kutokana na kwamba watu wetu hawana taaluma ya kuvitumia,” anaeleza.

“Rais wetu Dk John Magufuli ni mtu mwenye moyo wa huruma na shukrani, mwenye kutambua na kuthamini kazi nzuri inayofanywa, ndiyo sababu yake ya kutumia Kauli Mbiu ya ‘hapa kazi tu’ namuomba Rais wetu mpendwa atembelee Mang’ola ili apate kujionea kwa macho yake mwenyewe kazi na historia njema ya ufanisi inayofanywa na mapadri hawa,” anasema na kuongeza;

“Ninaiomba Serikali yetu ifanye marekebisho ya kimfumo ili kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa vibali kwa watu wa mataifa mengine wenye nia njema ya kuisaidi nchi yetu.”

Anasema kupitia kwa viongozi hao wa dini wamefanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye eneo la Mang’ola yenye thamani ya sh5,973,661,000 ikiwemo ujenzi wa madarasa 40 ya shule za msingi zilizotumia sh400.5 milioni, ujenzi wa Nyumba 35 za walimu sh350.7 milioni, ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana sh2.3 milioni, ujenzi wa ukumbi na ofisi nne za vijiji na nne za kata sh85 milioni.

Anasema ukarabati wa shule 11 za msingi kwenye Tarafa ya Mang’ola sh301.5 milioni, ujenzi wa Kituo cha afya sh1.2 bilioni, ufadhili wa fedha za uendeshaji wa kituo cha afya kila mwaka sh160.6 milioni, kukarabati kituo cha polisi sh3.1 milioni na kuchangia ujenzi wa msikiti sh25.8 milioni.


Pia, wamefanikisha ujenzi wa nyumba tano za watu wasiojiweza kwa gharama ya sh25 milioni, ununuzi wa trekta na vifaa vyake kwa CBO ya WAVIU sh62.8 milioni, kuhudumia kikundi cha wazee, wajane na wagane 25 sh23.4 milioni na kujenga ukumbi na bwalo la magereza sh25 milioni, ununuzi wa vitabu vya shule za msingi Tarafa ya Mangola sh75.3 milioni.

Anasema wamefanikisha ununuzi wa madawati kwa shule za msingi kwenye tarafa hiyo sh75 milioni, ujenzi wa mradi wa maji ambapo kuna mtandao wa miundombinu wenye umbali wa Kilometa saba sh300.7 milioni, ununuzi wa vitabu vya shule nne za sekondari kwa mwaka 2016 sh30.1 milioni, ujenzi wa kanisa katoliki lenye uwezo wa kuingia watu 1,500  sh1.800 bilioni.

“Pia kuna ujenzi wa makanisa matano katika vigango sh250.5 milioni, ujenzi wa kituo cha masista wafanyao kazi za afya na shuleni sh180.6 milioni, ujenzi wa karakana ya mafunzo ya useremala kwa vijana sh21.9 milioni, ununuzi wa vifaa katika karakana ya useremala sh200.6 milioni,” anasema Ole Mukusi.

Anasema pia ujenzi wa Kituo cha mafunzo kwa wasichana sh62.9 milioni, ujenzi wa maghala 12 ya kuhifadhia vitunguu katika vijiji saba sh180.8 milioni, kuwasomesha vijana 55 chuo kikuu sh125.9 milioni, vyote vimegharimu zaidi ya sh5.9 bilioni, ikiwa ni michango ya watu wa Hispania kwa watanzania muda ambao mapadre hao wamefanya kwenye parokia yao Mang’ola.

Anasema kwa muda waliofanya kazi Parokia ya Mang’ola mapadre hao Pepe na Miguel wamewezesha miradi hiyo iliyogharimu fedha hizo shilingi 5,973,661,000  ambayo ni michango ya watu wa Hispania kwa Watanzania waliopo Tarafa ya Mang’ola.

No comments:

Post a Comment