Thursday, 12 January 2017

LOSOITO WAPATIWA MAJI NA TANZANITEONE

Kaya 277 za wananchi 1767 wa Kijiji cha Losoito, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wenye tatizo kubwa la ukosefu wa maji, wanatarajia kuondokana na changamoto hiyo baada ya kampuni ya TanzaniteOne kuwapatia maji.
 
Ofisa mahusiano wa kampuni ya madini ya Tanzanite ya wilayani humo TanzaniteOne Halfan Hayeshi akizungumza alisema hivi sasa mradi huo umefikia asilimia 85 ili umalizike na kuzinduliwa ila wanachi wanapata maji.
 
Hayeshi alisema wananchi wa eneo hilo wanaendelea kupata huduma ya maji ila mradi kamili haujakamilika kwani wanahitaji kuweka mabomba urefu wa mita 500 ili kufikisha maji hayo karibu zaidi na jamii eneo la shule ya msingi Losoito.
 
“Tunatarajia kuweka mabomba ya urefu wa mita 500 ili kufikisha mradi huu karibu zaidi, ila hivi sasa wananchi wanapata huduma hiyo ya maji kwani awali tuliambiwa tufikishe mradi huo kwenye eneo la sasa ulipo,” alisema Hayeshi.
 
Alisema wanatarajia kuzindua mradi huo hivi karibuni baada ya kuwapa taarifa Katibu tawala wa mkoa huo Eliakim Maswi na mkuu wa wilaya hiyo Zephania Chaula, ambao ndiyo wataukabidhi kwa wananchi wa kijiji hicho cha Losoito.
 
Alisema mifugo na jamii ya eneo hilo hivi sasa wanafaidika na huduma hiyo ya maji na mara baada ya kununuliwa kwa rola sita za mabomba ya maji yatakayoweza kuwekwa katika mita 500 zilizobaki yatafika kwenye shule hiyo.
 
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho Ngatayai Mollel alishukuru uongozi wa kampuni ya TanzaniteOne kwa kufanikisha mradi huo wa maji, utakaowasaidia wananchi wa eneo hilo, ambao kwa muda mrefu walikuwa wanakabiliwa na tatizo la maji.
 
Mollel alisema kijiji hicho kilichoanzishwa mwaka 2009 hivi sasa kina wakazi 1767 chenye kaya 277 kilikuwa na wakati mgumu wa kupata huduma ya maji ila hivi sasa wananchi wameondokana na changamoto ya maji iliyowasumbua.
 
Hata hivyo, alitoa ombi la wananchi wa eneo hilo kujengewa zahanati kwani inawalazimu kutembea umbali mrefu kupata huduma ya afya pindi wanapougua hivyo kuwa tatizo hasa kwa wanawake na watoto.
 
Mmoja kati ya vijana wanaolinda mradi huo wa maji ili mabomba yasiibiwe Daniel Solomon, alisema wamepeana zamu ya kulinda kila siku watu watatu ili miundombinu isiharibiwe na jamii ya eneo hilo ifaidike na maendeleo hayo.
 
“Wakina mama walikuwa wanatembea umbali mrefu wa kilomita 20 kila siku kwenda na kurudi mji mdogo wa Mirerani, kwa kutumia wanyamakazi punda, ila hivi sasa wanaondokana na tatizo hilo la muda mrefu,” alisema Solomon.
 

No comments:

Post a Comment