Wananchi wanyonge ambao ni kaya masikini wamenufaika baada ya Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, George Bajuta, kujitolea
sh1.8 milioni kwa ajili ya kuzilipia kaya masikini 36 za watu 216 wa Kata ya
Simbay kwenye mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa (iCHF).
Bajuta ambaye ni
diwani wa kata hiyo aliyasema hayo kwenye uzinduzi wa mfuko wa afya ya jamii
ulioboreshwa (iCHF) ulioandaliwa na mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF)
mkoani humo na kudai kuwa kila kitongoji kitatoa kaya tatu za wanyonge wasiojiweza.
Alisema kata yake
ina vitongoji 12 na kila kitongoji kitachagua kaya tatu ambazo ni familia
za wanyonge zisizojiweza ili awalipie sh30,000 kila kaya yenye watu sita, baba, mama na
watoto wanne, zitakazopata huduma za afya kwa mwaka mzima.
“Mimi sina
utajiri mkubwa ila nimeamua kujitolea kidogo nilichonacho kwa kuhakikisha wale
ndugu zangu wanyonge wasiokuwa na uwezo kabisa kwenye kila kitongoji nao wapate fursa ya
kutibiwa bure kwa mwaka,” alisema Bajuta.
Mkuu wa wilaya
hiyo Sarah Msafiri akizungumza wakati akizindua mfuko huo alisema wananchi wa
eneo hilo wanapaswa kushiriki ipasavyo kwa kujiunga na (iCHF) kwani hadi mwisho
wa mwaka inatakiwa asilimia 50 ya watu wajiunge.
“Hapa kwenye Tarafa
ya Simbay kuna zaidi ya wakazi 6,200 hivyo tunapaswa kujiunga kwa wingi ili watu
zaidi ya 3,100 ambayo ndiyo nusu ya watu ili kutimiza lengo la serikali la
kuhakikisha hadi idadi hiyo inafika,” alisema Msafiri.
Meneja wa mfuko
wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoani Manyara, Isaya Shekifu alisema kila kaya
itakayotoa sh30,000 kwa ajili ya kuchangia mfuko huo nayo serikali kuu
huchangia nusu nyingine sh30,000 na kuwa sh60,000.
Shekifu alisema iCHF
iliyoboreshwa inajenga mfuko endelevu wa kuchangia kijamii gharama za matibabu
na kuboresha ubora wa huduma za afya kupitia mafunzo kwa watoa huduma, utoaji
vifaa tiba na uboreshaji miundombinu ya huduma.