WACHIMBAJI wawili
haramu wamenusurika kufariki dunia baada ya kuishia hewa walipoingia kwa wizi
kwenye mgodi wa kampuni ya TanzaniteOne ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara.
Akizungumza
na waandishi wa habari, kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi
(ACP) Francis Massawe alisema wachimbaji hao haramu waliingia kwenye mgodi wa
TanzaniteOne uitwao Investa.
Kamanda Massawe
alisema tukio hilo lilitokea juzi alasiri kwenye mgodi huo baada ya wachimbaji
hao kuingia kwa wizi chini kwa chini mgodini kupitia mitobozano na kufanya kazi
kwenye mgodi huo ambao hautumiwi hivi sasa.
Aliwataja
wachimbaji hao haramu ambao walinusurika kufariki dunia kwa kukosa hewa mgodini
ni Ramadhani Juma na Mohamed Jumanne wote wakazi wa mji mdogo wa Mirerani
wilayani Simanjiro.
Alisema
wanawashikilia watu hao wawili kwa ajili ya mahojiano kabla ya kuwafikisha mahakamani
kujibu tuhuma za kuingia kwa jinai kwenye mgodi ambao hawaumiliki wana
hawafanya kazi katika mgodi huo.
Hata hivyo,
alitoa onyo kwa watu wote wanaowafadhili wachimbaji hao haramu kuzamia bila
halali kwenye mgodi wa kampuni hiyo kwani vitendo hivyo huchangia uhalifu
kutokana na kufanya kazi eneo ambalo hawalimiliki.
Ofisa uhusiano wa
kampuni ya TanzaniteOne Halfan Hayeshi alisema siku ya tukio hilo watu 10
waliingia kwenye mgodi huo wa Investa ambao haufanyiwi kazi kupitia mtobozano
uliopo na kuendelea na shughuli zao bila halali.
Hayeshi alisema
baada ya kuishiwa hewa kupitia mashine ya jenereta iliyokuwa inatoa hewa ya chafu
ya ukaa, watu hao walitoa taarifa kwa mlinzi wa kampuni hiyo ambaye aliwaambia
wasubiri atoe taarifa kwa uongozi ndipo wakatoroka.
“Baada ya kufika
eneo la tukio tulitoa taarifa polisi na uongozi wa ofisi ya madini Mirerani
ndipo tukaanza zoezi la kuwaokoa watu hao ambao tuliwakuta wawili wakiwa na
hali mbaya na hadi sasa wanashikiliwa na polisi,” alisema.