Saturday, 11 June 2016

WAANDISHI WA MANYARA WAJENGEWA UWEZO KUANDIKA HABARI ZA INTANETI



Waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara, wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya intaneti kwa uandishi wa habari wa kisasa kwa ajili ya kutafuta habari, mawasiliano ya mtandao, kuchapisha habari makazini mwao.
Kaimu mkurugenzi wa Taasisi ya vyombo vya habari kusini mwa bara la Afrika, tawi la Tanzania, Andrew Marawiti, akizungumza jana mjini Babati alisema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa matumizi sahihi ya intaneti.

Marawiti alisema mafunzo hayo yatawasaidia kutambua usalama wa teknolojia ya habari na umuhimu wake kwa waandishi, matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, umuhimu wa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa intaneti.  
“Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Misa Tan kwa kushirikiana na mfuko wa vyombo vya habari, mawasiliano na maendeleo Finland Vikes Foundation kwa msaada wa Wizara ya mambo ya nje ya Finland,” alisema Marawiti.



Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo Seif Jigge alisema hayo ni mafunzo ya tatu kuyatoa kwa waandishi wa habari, kwani awali aliwaongezea uwezo wa habari za intaneti waandishi wa mikoa ya Mtwara na Kilimanjaro.

Jigge alisema kupitia mafunzo haya waandishi hao watakuwa na uwezo zaidi wa kupata taarifa zao kupitia vyanzo husika na kutambua namna ya kuhifadhi kwa usalama kwenye mafaili yaliyopo katika kompyuta ili zisivamiwe na virusi.



Mmoja kati ya mwandishi aliyeshiriki mafunzo Restituta Fissoo alisema alijifunza kupata habari kwenye vyanzo vya uhakika ikiwemo takwimu au habari za wizara kuliko kutafuta katika mitandao ya vyanzo visivyo na uhakika.

Mwandishi mwingine Baraka Ole Maika, alisema amejifunza mengi kupitia mafunzo hayo ikiwemo namna ya kuhifadhi taarifa zake kwa usalama zaidi, kufahamu teknolojia ya habari kwa upana wake na kupata anuani ya vyanzo vya habari.  

MAWAKALA WA PEMBEJEO MANYARA WATAKIWA KUWAJALI WAKULIMA


Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi amewataka mawakala wa pembejeo za kilimo wa mkoa huo, kuhakikisha wanazitoa huduma zao vyema kwa wakulima wa wilaya zote, ili waweze kujinyanyua kiuchumi.

Maswi alitoa agizo hilo mjini Babati, wakati akizungumza kwenye mapokezi ya vocha za ruzuku zilizobaki katika halmashauri za wilaya zilizopo katika mkoa huo kwa upande wa msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016.  

Aliwataka mawakala hao watoe taarifa kwake kwenye vikwazo vya kufanya biashara ya pembejeo za kilimo na endapo watendaji wa serikali watakuwa wanawataka wawape asante, wafikishe suala hilo ili wawachukulie hatua.

“Tunapaswa kutumia uzalendo jamani kwani hii nchi ni yetu na tutakaoijenga ni sisi wenyewe na pia tutakaoibomoa ni sisi sisi, hivyo tujipange kumsaidia mkulima wa kawaida katika kupata maendeleo ya kilimo,” alisema Maswi.

Alisema atawapa ushirikiano mawakala wote wa pembejeo ili kuhakikisha mkoa wa Manyara, unaendelea kupiga hatua katika suala zima la kilimo na wakulima wananufaika kupitia pembejeo watakazopatiwa msimu wa kilimo.

Hata hivyo, amewataka mawakala hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo kwani mkoa huo upo nyuma kimaendelea kwenye mambo mengi na kupitia kilimo wananchi wengi wataweza kupiga hatua kubwa tofauti na awali.

Kwa upande wake, ofisa kilimo wa mkoa wa huo, Coletha Shayo alisema halmashauri ya Babati mjini walibakiza vocha 1,157 za thamani ya sh34.865 milioni, Babati vijijini vocha 4,329 zenye thamani ya sh119.500 milioni.

Shayo alisema Hanang’ ilibakiza vocha 1,800 za sh54 milioni, Kiteto vocha 13,650 za sh407 milioni, Simanjiro vocha 5,943 za sh164.135 milioni, Mbulu vijini vocha 10,800 za sh225.645 milioni na Mbulu mjini vocha 7,589 za sh224 milioni.

Wednesday, 8 June 2016

WAZIRI LUKUVI AZINDUA BARAZA LA ARDHI NA NYUMBA KITETO



Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, William Lukuvi amezindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, ambalo kwa kiasi kikubwa litamaliza migogoro ya ardhi iliyokuwa inawakabili wananchi wa eneo hilo.

Awali, wananchi wa wilaya hiyo iliwabidi wafuate huduma hiyo umbali wa kilometa 300 kwenda na kurudi wilayani Simanjiro ambapo kuna baraza kama hilo, ili kufungua mashauri yao kwenye masuala ya ardhi au nyumba.

Akizungumza wilayani Kiteto wakati akizindua baraza hilo, Lukuvi alisema baraza la Kiteto na Lushoto ni miongoni mwa mabaraza 47 yatakayozinduliwa hivi karibuni kwenye wilaya mbalimbali ambazo hazina mabaraza.



Alisema baraza hilo litawasaidia wananchi wa Kiteto kuondoa kero ya kufuata huduma hiyo wilayani Simanjiro kwani kati ya kesi 150 zinazofanyika kwa mwaka wilayani Simanjiro, kesi 100 zinawahusu watu wa wilaya ya Kiteto.

“Lengo la serikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli ni kumaliza migogoro ya ardhi hivyo kupitia haya mabaraza ya ardhi na nyumba na katika vijiji tutaweka matumizi bora ya ardhi ili kusiwepo na migogoro,” alisema Waziri Lukuvi.

Alisema mpango wa matumizi bora ya ardhi utasababisha wakulima na wafugaji kutogombana kwani kila kijiji kitatenga eneo la mashamba, malisho ya mifugo, makazi, sehemu za ibada na huduma nyingine na kuondokana na migogoro.


Mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera alisema baraza hilo litasaidia kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi iliyokithiri kwani awali wananchi wengi walikuwa wanafika mjini Babati kutoa malalamiko yao ya migogoro ya ardhi. 

Hata hivyo, Dk Bendera aliwataka Mwenyekiti wa baraza hilo la Kiteto Charles Mnzava na wazee wa baraza kutenda haki kwa wananchi wa Kiteto wakati wa kuendesha mashauri hayo ili jamii ione faida ya kuwepo kwa baraza hilo.

“Sasa wananchi waliokuwa wanakwenda Simanjiro kuhudumiwa wamerahisishiwa kwa kuletewa baraza hapa Kiteto ila isiwe njia ya kupokea rushwa na kuwa kero kwa jamii, tendeni haki ili watu waridhike,” alisema.

Mbunge wa jimbo la Kiteto, Emmanuel Papian alimshukuru Waziri Lukuvi kwa kuzindua baraza hilo kwani litasaidia kwa namna moja au nyingine kumaliza migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa imekithiri kwenye eneo hilo la Kiteto.

“Kupitia baraza la ardhi na nyumba hapa Kiteto huu ndiyo utakuwa mwisho wa kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwani awali tulikuwa tunateseka kwenda Simanjiro kwani jamii ilikuwa inatumia gharama kubwa,” alisema Papian.

Alitoa ombi kwa Waziri Lukuvi kusaidia upimaji wa viwanja vyote vya wilaya hiyo ili uwekwe kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi, kwani huo utakuwa mwisho wa migogoro yote ya ardhi iliyokuwa imekithiri Kiteto.