Thursday, 24 December 2015

WACHIMBAJI TANZANITE KUANDAMANA KUPINGA MIGODI YAO 19 KUSIMAMISHWA KAZIWachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro wameazimia kufanya maandamanao ya amani kupinga kusimamishwa kufanya kazi migodi yao 19 iliyopakana na kampuni ya TanzaniteOne.

Wachimbaji hao waliazimia kufanya maandamano hayo ya amani mapema mwezi ujao na wanatarajia kuwa yatapokelewa na mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera, wakipinga kunyanyaswa na kufungiwa kwa migodi yao 19.

Mmoja kati ya wachimbaji hao, Omary Mandari alisema suluhisho la manyanyaso kwa wachimbaji wadogo litamalizwa endapo wataandamana kwa amani kupinga unyanyasaji huo kwani migodi hiyo 19 imefungiwa kwa makosa.

“Tutaandamana kwa amani kuanzia shamba la Maro na kuzungukia kwenye baadhi ya barabara za Mirerani hadi getini mnadani, kwa lengo la kuonyesha ulimwengu kuwa tunapinga migodi yetu 19 kusimamishwa,” alisema Mandari.Makamu Mwenyekiti wa Marema Wariamangi Sumari alisema maandamano hayo ya amani yatajumuisha wachimbaji wadogo, wafanyabiashara na wakazi wote wa Mirerani kwani maisha yao yanategemea madini ya Tanzanite.

“Maandamano hayo yatakuwa ya halali kabisa kwani tutaomba kibali kwa mkuu wa polisi wa wilaya (OCD) na kumtaarifu mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa aje hapa Mirerani kwa ajili ya kupokea maandamano hayo,” alisema Sumari.

Mwenyekiti wa Minasco Charles Mlay, alisema wachimbaji wadogo wamekuwa wananyimwa haki zao bila sababu ya msingi hadi kusababisha migodi 19 kusimamishwa kimakosa ili hali wanachimba kihalali migodi yao.

“Hakuna mtu aliye juu ya sheria kila wakati wachimbaji wadogo wananyanyasika kwa kunyimwa haki zao wakati wanachimba kihalali hivyo ni bora kufanya maandamano ya amani yatakayoeleza hisia zetu,” alisema Mlay.Katibu wa Marema Abubakari Madiwa alisema azimio hilo la kuandamana kwa wachimbaji hao wadogo linaandaliwa ipasavyo ikiwemo kamati ndogo itakayoratibu mpango wote hadi kufanikisha maandamano hayo ya amani.

Zephania Joseph alisema haki ya wachimbaji wadogo haiombwi inadaiwa, hivyo huu ni wakati muafaka wa kuungana kwa wachimbaji hao kufanya maandamano ya amani ili kufikisha kilio cha kwa migodi yao 19 kusimamishwa.


No comments:

Post a Comment