Monday 21 December 2015

TANZANITE YENYE THAMANI YA BILIONI 2.6 YAKAMATWA KIA



KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Omar Chambo amesema thamani ya madini ya tanzanite yaliyokamatwa yakitoroshwa nje ya nchi bila kuwa na vibali hivi karibuni kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) imefikia Dola za Marekani 1,207,990 (Sh bilioni 2.6).

Alisema hayo jijini Arusha wakati wa kikao chake na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya tanzanite na kufuatilia kwa karibu shughuli za uchimbaji na biashara ya madini hayo ili yanufaishe taifa.

Alisema tanzanite hiyo ghafi yenye uzito wa gramu 2,015.59, ilikuwa ikitoroshwa na raia wa India, Jain Anurag aliyekuwa akitaka kwenda mji wa Jaipur kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Qatar wiki iliyopita.



Alisema madini yaliyokamatwa yameshataifishwa kama ambavyo sheria na kanuni za madini zinavyoelekeza na kwamba ukamataji dhidi ya watorosha madini hufanywa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Wakala wake wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji.

Aidha, amesema Serikali itafuta leseni za wafanyabiashara wa madini watakaobainika kutorosha rasilimali hiyo nje ya nchi ikiwemo kuwakamata wachimbaji na wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi stahiki kwa serikali.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla ametoa saa 24 kwa raia wa kigeni wote wanaojihusisha na biashara ya madini ya tanzanite na madini mengine kinyume cha sheria, kuondoka nchini mara moja na watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments:

Post a Comment