Sunday, 13 December 2015

MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA (NHIF) YATOA MSAADA WA MASHUKA 100 BABATI



Hospitali ya Mji wa Babati Mkoani Manyara, (Mrara) ambayo inakabiliwa na upungufu wa mashuka, imekabidhiwa msaada wa mashuka 100 na Mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) kwa ajili ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo.

Msaada huo wa mashuka 100 ulikabidhiwa juzi kwa mkuu wa wilaya ya Babati Crispin Meela na Meneja wa NHIF mkoani Manyara Isaya Shekifu, ambaye aliahidi kuongeza mashuka mengine 150 hivi karibuni kwenye hospitali hiyo.

Alisema wametoa msaada huo mara baada ya kutembelea hospitali hiyo na kubaini upungufu mkubwa wa mashuka yanayotumiwa na wagonjwa wanaolazwa kwenye wodi za hospitali hiyo ya Mrara.

“Baada ya kutoa mashuka haya 100, hivi karibuni tunatarajia kutoa mashuka mengine 150 ili yawe 250 ambayo kwa kiasi kikubwa yatamaliza changamoto ya ukosefu wa mashuka kwa wagonjwa wa hospitali hii,” alisema Shekifu.

Alisema wametoa msaada huo mara baada ya kutembelea hospitali hiyo na kubaini upungufu mkubwa wa mashuka yanayotumiwa na wagonjwa wanaolazwa kwenye wodi za hospitali hiyo ya Mrara.



Meela akizungumza mara baada ya kupokea mashuka hayo, aliushukuru uongozi wa NHIF mkoani humo ambao walichukua muda mfupi wa kutoa msaada huo mara baada ya kubaini kuwa kuna tatizo la upungufu wa mashuka.

Alisema hivi karibuni yeye na Shekifu walitembelea hospitali hiyo na kukuta kuna tatizo kubwa la upungufu wa mashuka kwa wagonjwa na alipotoa ombi hilo lilikubaliwa na kutekelezwa kwa muda mfupi hivyo anawapongeza NHIF.



Nao, baadhi ya wakazi wa mji wa Babati walitoa ombi kwa asasi, taasisi, makampuni na mashirika ya serikali na ya binafsi, kuiiga NHIF na kutoa mashuka mengine kwenye hospitali hiyo ambayo ina uhaba wa mashuka kwa wagonjwa.

No comments:

Post a Comment