Wakazi wa Wilaya ya
Kiteto, Mkoani Manyara, wametakiwa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) ili
waweze kupatiwa matibabu kwa kuchangia sh10,000 na kupatiwa matibabu mwaka
mzima kwa kaya yenye watu sita.
Akizungumza kwenye
kijiji cha Engusero wakati wa uzinduzi wa uhamasishaji wa kaya kujiunga na CHF,
mkuu wa wilaya hiyo Kanali Samuel Nzoka alisema kaya nyingi zikijiunga ndiyo
upatikanaji wa dawa unakuwepo.
Kanali Nzoka alisema
tatizo la ukosefu wa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitalini
litamalizika, endapo kaya nyingi zikijiunga na CHF kwani serikali nayo itaweka
mkono wake ili kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa.
Wakati wa uzinduzi wa
zoezi hilo Kanali Nzoka alijitolea sh20,000 kwa ajili ya kuzilipia kaya mbili
za watu 12 wa kijiji cha Engusero na Dosidosi na kuungwa mkono na viongozi
wanne wa wilaya hiyo waliojitolea sh10,000 kwa kila mmoja.
Meneja wa mfuko wa
Taifa wa Bima ya afya (NHIF) wa mkoa wa Manyara, Isaya Shekifu alisema
mwanachama wa CHF atanufaika na huduma zote za afya za msingi na kinga na tiba
kwa zahanati, kituo cha afya na hospitali.
Shekifu alitaja
baadhi ya huduma zinazotolewa ni vipimo vya maabara, wagonjwa wa kutwa na
kulazwa, upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na halmashauri husika na
wanachama kupata huduma bora ya afya kwa
mwaka.
“Pia watapata huduma
ya upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na Halmashauri zinazoendesha
mifuko hii zinapata mapato ya tele kwa tele kutoka serikalini ambayo yatatumika
kuboresha huduma za afya,” alisema.
No comments:
Post a Comment