Thursday, 23 October 2014

WAZAZI KITETO WAZALISHWA KWA KUTUMIA MIFUKO YA PLASTIKI KKwa hisani ya gazeti la Mwananchi la Alhamisi ya Octoba 22 mwaka 2015

Joseph Lyimo, Mwananchi

Kiteto.Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni. Haya ndiyo yanayojiri katika Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara ambako baadhi ya wakunga wa jadi huvaa mifuko ya plastiki maarufu kama ‘rambo au malboro’, mikononi ili kuwahudumia kina mama wakati wa kujifungua.

Awali wakunga hawa ambao hufanya kazi hii pasipo malipo yoyote rasmi, walikuwa wakizalisha wajawazito bila ya kuvaa chochote, lakini walianza kutumia aina hiyo ya ‘kinga’, baada ya wenzao wawili kuambukizwa Virusi vya Ukimwi.

Rose Mary Loshiye, ambaye pia ni mkunga wa jadi, anasema: “Wakunga wa jadi walikuwa wakiwazalisha wanawake wa jamii ya wafugaji bila kuvaa mipira mikononi na baadhi yao waliambukizwa Ukimwi, kwa hiyo tangu wakati huo hakuna anayethubutu kuzalisha akiwa mikono mitupu.

“Ikiwa hawana mipira ya kuvaa mikononi wanatumia mifuko ya plastiki, wanajifunga mkononi halafu wanatoa huduma hiyo kwa wakinamama.”

Wilaya hii inakaliwa zaidi na jamii ya wafugaji na huduma za afya na tiba zikipatikana umbali wa kati ya kilometa 45 na 50, hali ambayo inawapa wakunga wa jadi nafasi muhimu ya kuwa wahudumu pekee kwa wanawake wanaojifungua hasa nyakati za usiku.

Huduma ya afya kwenye Wilaya ya Kiteto yenye kata 19 na vijiji 59, ni changamoto kubwa kwani haikidhi matakwa ya sera ya taifa ya afya ya 2007 inayotaka kila kata iwe na kituo cha afya na kila kijiji kiwe na zahanati.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Bosco Ndunguru anasema Kiteto yenye kilometa 16,685 za mraba, ina hospitali moja ya wilaya na vituo viwili tu vya afya kati ya 15 vinavyohitajika na ina zahanati 15 kati ya 59 zinazotakiwa.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2012, Kiteto ina watu 244,669 wakiwemo wanaume 120,233 na wanawake 124,436 na ongezeko la watu ni wastani wa asilimia 6.1 kwa mwaka na kila kaya ikikadiriwa kuwa na wastani wa watu watano.

Vifaa kwa wakunga

Mkunga wa jadi wa Kijiji cha Bwagamoyo wilayani humo, Amina Malekela (56) anasema tatizo kubwa ni uhaba wa vifaa na kwamba wanapouliza sababu za kutopatiwa vifaa hivyo, wanaelezwa kuwa hawatambuliwi na hawapaswi kusaidia kuzalisha.

“Mara nyingi wanawake wengi hujifungulia nyumbani kupitia wakunga wa jadi ambao wanatumia mikono mitupu kuzalisha, kwani mipira ni tatizo haipatikani,” anaeleza Malekela.

Anasema kwa kuwa matukio hayo huwa ya ghafla, wakunga hushindwa kuvaa hata hiyo mifuko ya plastiki ambayo hutumia kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya VVU na kwamba ndiyo sababu wenzao wawili waliambukizwa.

Mratibu wa afya ya uzazi na mtoto wilayani Kiteto, Helena Batroba alithibitisha wakunga wawili wa jadi kufikishwa hospitalini wakidaiwa kuwa na maambukizi ya VVU.

“Kuna wanawake wawili ambao mwaka 2010 walikuwa wanatibiwa hapa hospitali ya wilaya, wakiwa na virusi vya Ukimwi na tulipouliza tukaelezwa kuwa ni wakunga wa jadi, ila sikumbuki walikuwa wametoka maeneo gani, mmoja alikuwa na miaka 70 na mwingine miaka 65,” anasema Batroba.

Kwa upande wake, Loshiye anasema licha ya kwamba hawana vifaa vya kazi hiyo, wamekuwa wanafanya kazi yao bila kulipwa chochote, kwani wanafanya hisani.

Anaeleza kwamba wakunga wa jadi hawana gharama kubwa kwa kuwa hupatiwa asante ya mdomo na wao huridhika kwa moyo mmoja na wakati mwingine hupewa kanga, vitenge na karanga.

Loshiye anasema wengine huridhika kwa kupata sifa wanapozalisha wanawake salama bila madhara yoyote.

Diwani wa Kata ya Magungu, Daudi Mwedimwage anasema wakunga wa jadi wanategemewa na wanawake wengi wajawazito katika kuwazalisha kutokana na huduma za afya kuwa mbali na kata hiyo.

“Kutoka hapa Magungu hadi Kibaya makao makuu ya wilaya ambapo kuna hospitali kilomita 55, na kutoka Magugu hadi kule Makawa wilayani Kongwa mkoani Dodoma ni kilomita 45, hivyo inakuwa vigumu jamii kupata huduma za afya kutokana na umbali,” anasema Mwedimwage.

“Kwa hiyo ni kweli kwamba wakunga wa jadi wanatumia mifuko ya malboro kwa ajili ya kupokea watoto wakati wa kuzalisha na hiyo inatokana na ukosefu wa vifaa vya kitaalamu, hivyo inawabidi watumie namna za kienyeji kwa ajili ya kujinusuru na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwani hawana namna nyingine.”
Hospitali ni gharama

Mkazi wa Kijiji cha Partimbo wilayani humo, Paulina Kimani (39) anakiri kwamba huzalishwa na wakunga wa jadi kutokana na ukubwa wa gharama za kujifungua kwenye hospitali ya wilaya hiyo ambazo ni kuanzia Sh20,000.

“Tunashindwa kuchangia hizo fedha tunazoelezwa kwamba ni za nyembe, gloves (mipira ya kuvaa mikononi), mpira wa kunyonyea uchafu na mpira wa kulalia wakati wa kujifungua,” anasema Kimani.

“Pia hao wahudumu wana lugha chafu, ni tatizo kwa mtoto mdogo anakwambia wewe mama hadi umri huu bado unazaa tu achia watoto wako au wajukuu wako. Unapenda starehe hadi umri huo?”

Hata hivyo, kaimu mganga mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Dk Leadry Malisa alikanusha wanawake wajawazito kutakiwa kutoa fedha kwa ajili ya kulipia huduma ya kuzalishwa kwenye hospitali au vituo vya afya na kwamba huduma hizo hugharamiwa na Serikali.

Dk Malisa anakiri upungufu wa vifaatiba, pia vifaa vya kujifungulia kwa wanawake wajawazito, kutokana na mgawo mdogo unaotolewa na Bohari Kuu la Dawa (MSD) na hiyo ni changamoto inayowakabili kwa muda mrefu wilayani humo.

“Suala la uchache wa mipira ya kuvaa mikononi (gloves) ni tatizo, haitoshi, hivyo tunawaomba kina mama hasa wa jamii ya wafugaji, wakikaribia kujifungua, wajiandae mapema kwa kusogea karibu na huduma za afya, ili wapate huduma sahihi wakati wa kujifungua kuliko hivi sasa wanapojifungulia nyumbani mwao kwa msaada wa wakunga wa jadi,” anaeleza Dk Malisa.

Kwa upande mwingine, mratibu wa afya ya uzazi na mtoto, Batroba anasema si kweli kwamba wauguzi katika sehemu za kutoa huduma za afya wanatoa lugha zisizo rafiki kwa wanawake wajawazito na kwamba kuna uadilifu mkubwa.

“Hata hivyo, tutachunguza suala hili kama kweli lipo, ila tumekuwa tukifuatilia jambo hili kwa wauguzi wetu na tumebaini kwamba lugha wanayotumia ni ya kitaalamu na siyo lugha ya matusi kama wanavyofikiri baadhi ya wanawake hao,” anasema Batroba.

Wakunga watetewa Katibu wa tiba asilia na tiba mbadala wa Wilaya ya Kiteto, Muya Kisairo anasema wakunga wa jadi ni muhimu wilayani humo kwani wamekuwa wakitoa huduma za uzazi, lakini Serikali ni kama haiwatambui kwa na hivyo haiwapi vifaa.

Kisairo anasema wilaya hiyo ina zaidi ya wakunga 100 wa jadi ambao wapo katika vijiji mbalimbali na kila kijiji kinawategemea katika kuwapa huduma wanawake tangu wakiwa wajawazito, kwa kuwa wengi wao wanashindwa kwenda kliniki au hospitalini kutokana na umbali.

Anaeleza kwamba utendaji kazi wa wakunga wa jadi wilayani humo ni mzuri isipokuwa tatizo ni ukosefu wa vifaa kwani baadhi ya maeneo ya vijijini hadi ufike kwenye huduma za afya, inakubidi utembee umbali wa maili 10 au zaidi, hivyo shughuli zote za uzalishaji wanafanya wakunga wa jadi.

“Upungufu wa vifaa tiba ni tatizo sana kwa wakunga wa jadi wa Wilaya Kiteto ambao ni wakombozi wa jamii linapokuja suala la uzazi, kwani wanatumia mifuko ya rambo kutokana na ukosefu wa mipira ya kuvaa mkononi,” anasema Kisairo.

No comments:

Post a Comment