Tuesday, 14 October 2014

MGOGORO MACHIMBO YA MADINI YA TANZANITE MIRERANI



Mussa Juma, Mwananchi

Mirerani. “Sheria hii inatumika kwenye machimbo ya dhahabu na almasi siyo tanzanite ambayo inachimbwa kwa kufuatwa miamba,” anasema Mnenei.

Anasema kwa kutaka kusimamia sheria hiyo ni kutaka kuwaondoa wachimbaji wadogo, Mererani kwani kwa jinsi walivyopewa maeneo yao hakuna hata mmoja ambaye anachimba ndani ya leseni.

“Kuwaondoa wachimbaji hapa ni kusababisha maafa kwa familia zao na taifa zima kwani watu zaidi ya 10,000 wakikosa kazi, sijui wao na familia zao watategemea nini,” anasema Mnenei na kuisihi Serikali kutatua mgogoro huo.

Papa King Mollel ni mmoja wa wachimbaji wadogo, maarufu Mkoa wa Arusha, anasema sheria hiyo ya madini na gharama kubwa za zana za uchimbaji ni kikwazo kwa wachimbaji wadogo.

“Ni kweli migodi mingi imesimama, lakini tatizo ni sheria na gharama za uchimbaji pia ni kubwa kwa sasa tofauti na miaka ya nyuma,” anasema.

Mbunge wa Simanjiro, Christopha Ole Sendeka anafafanua kuwa kimsingi sheria ya uchimbaji madini ya vito, ipo wazi kuwa madini hayo yatachimbwa na wazawa pekee sasa kuwa na sheria na kutetea mwekezaji ni kuvunja sheria pia.

“Msimamo wangu hautabadilika ni muhimu kuifanyika marekebisho sheria ya uchimbaji madini ya vito, ili iendane na wakati na sheria iliyopo sasa haitekelezeki,” anasema Sendeka.

Watafiti nao waeleza upungufu wa sheria

Amani Mustapha ni Mkurugenzi wa Shirika la Haki Madini, ambao wamefanya utafiti mbalimbali Mirerani, anasema sheria hiyo ya madini haitekelezeki na inalenga kuwaondoa wachimbaji wadogo Mirerani.

Anasema kwa sasa hakuna sababu za kulaumiana kwani, makosa yalifanyika tangu miaka ya nyuma kugawa machimbo ya Mirerani kisiasa na kutoa eneo moja kubwa kwa kampuni moja ya wawekezaji bila hata kuzingatia sheria ya madini.

Mustapha anasema ni muhimu busara kufuatwa, kwani wachimbaji wadogo wote zaidi ya 10,000 eneo lao halifikii eneo la mwekezaji mmoja.

“Binafsi nilikuwa mmoja wa wajumbe walioambatana na wachimbaji Dodoma kuonana na Kamati ya Bunge na tulieleza tatizo hilo kwa mapana na ambalo linasabisha sasa migodi mingi kusimama,” anasema.

Anasema kwa mapendekezo yake, ni busara sheria kutazamwa upya pia kupunguza eneo la mwekezaji ili wachimbaji wadogo wachimbe kwani wengi maisha yao yanategemea Mirerani.

“Ukiwaacha watu zaidi ya 10,000 bila ajira kwa kumlinda mtu mmoja, tutarajie matukio mengi ya ajabu mijini na ongezeko la uhalifu,” alisema.

Alisema machimbo ya Mirerani yanategemewa na zaidi ya watu 40,000 wa Wilaya ya Simanjiro na Mkoa wa Arusha, hivyo kuwabana wachimbaji wadogo kutakuwa na athari kubwa kama ambazo zimeanza kuonekana sasa kuzorota kwa uchumi wa Mirerani.

Mustapha anasema kutokana na majibu ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa wachimbaji wadogo muafaka hadi sasa haujapatikana na suala hili sasa limepelekwa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Mchimbaji Ismail Kaaya anasema pia kupewa mwekezaji mmoja kumiliki eneo la kilomita za mraba 7.6 ni makosa kwa mujibu wa kanuni za uchimbaji madini ya vito aya ya 5(1)(f) ambayo inasema ukubwa wa mwisho wa eneo utakuwa kilomita moja ya mraba.

“Pia hata hii sheria ambayo imesababisha migodi kufungwa ilikuwa haituhusu sisi kwani imetungwa wakati tayari tumekuwa tumeingia chini eneo hilo la mwekezaji kwa kuwa hakukuwa na sheria za kuzuia kutoingiliana chini ya migodi,” anasema.

Lusekelo Mwakalukwa ni mmoja wa wanasheria wa Kampuni ya Tanzanite One, anaeleza uvamizi ambao unafanywa na wachimbaji wadogo katika migodi ya Tanzanite One ni kukiuka sheria na umesababisha madhara kadhaa kwa wafanyakazi.

Hali ya uchimbaji Mirerani

Ofisa madini ambaye ni mtaalumu wa miamba (jiologist) Mererani, Mithayo Fransis kati ya migodi 551 inayochimbwa katika maeneo ya kitalu B na D ni migodi isiyozidi 120 ambayo ndiyo inachimbwa kwa sasa. 

Hata hivyo, anasema licha ya sheria hiyo, lakini kuna matatizo mengine yanayochangia kusimamishwa uchimbaji hasa ni gharama kubwa za uchimbaji kwa sasa kutokana na migodi mingi kufika umbali mrefu.

“Ndiyo sababu sasa hata wafanyakazi wamepungua sana mgodi ambao ulikuwa una vijana kati ya 200 hadi 100 sasa una vijana 15 tu, kwani kuna migodi imeanza kutumia zana za kisasa katika kutoa nje michanga tofauti na zamani kutumia watu,” anasema.

Anapinga pia hoja kuwa madini mengi yapo, eneo la mwekezaji kitalu C kwa maelezo kuwa mserereko wa miamba ya madini haiwezi kuwa sawa kwa migodi ya kitalu B na D yote kudai miamba inaelekea kitalu C.

Maelezo ya Wizara ya Nishati na Madini

Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane licha ya kukiri siasa ndiyo ilivuruga ugawaji wa vitalu Mirerani, lakini anasema ni muhimu sheria kufuatwa.

Anasema siyo kweli kuwa wizara ilitunga sheria hiyo, kumlinda mwekezaji kwani sheria ilikuwepo tangu mwaka 1998 na kilichofanyika mwaka 2004 na 2010 ni kuitafrisi vizuri sheria.

Magayane anafafanua kuwa haiwezekani mtu mwenye leseni ya madini kuchimba madini nje ya leseni, kwani jambo hilo halipo duniani na hakuna ukiukwaji wa sheria kutokana na msimamo wa wizara hiyo.

Anasema ni kweli kuwa kugawa migodi kwa mita 50 kwa 50 ilikuwa ni makosa kwani eneo hilo, huwezi kuchimba madini na ni kinyume cha sheria.

Magayane anasema tatizo na uchimbaji kwa wachimbaji wengi wadogo siyo endelevu kwani wamekuwa wakutumia fedha nyingi kufuata eneo ambalo wamepata taarifa kuna madini bila kujali ukubwa wa leseni.

“Ni kweli migodi mingi ipo ndani ya eneo la mwekezaji Tanzanite One na ndiyo sababu tulitaka kuifunga migodi 19 na kuibua malalamiko na jambo hili ni la kisheria,” anasema.

Anasema pia inawezekana kufungwa kwa migodi mingi ya wachimbaji wadogo kunatokana na maeneo yao kuisha madini na hili lipo kwa migodi mingi nchini.

Nini kifanyike Mirerani kunusuru wachimbaji wadogo

Ili kutowaondoa maelfu ya wachimbaji wadogo Mirerani, Kamishna Mahayane anaungana na Waziri Muhongo, kuwashauri wachimbaji wadogo kuungana na kuunda kampuni moja ili wao na wawe wanagawana mapato.

Takwimu za wizara hiyo zinaonyesha kama wachimbaji 100 wenye hisa wakiungana kila mmoja anaweza kupata takriban Sh500 milioni kwa mwaka kutokana na makisio yaliyofanyika kwa mapato ya Dola 35 milioni kwa mwaka Mirerani.

Anasema kwa uchimbaji wa sasa unachochea migogoro na ni vigumu kuendelea kwa muda mrefu kwani kunahitajika teknolojia za kisasa zenye gharama kubwa kama wasipoungana.

Hata hivyo, ushauri huu ambao ni wa muda mrefu wa Serikali unapingwa na wachimbaji kwa maelezo ya tofauti kubwa ya uwekezaji katika migodi baina yao.

“Kuna mtu amewekeza zaidi ya Sh8 bilioni sasa kumwambia aanzishe kampuni moja na mtu ambaye hajawekeza hapa ni tatizo pia tunadhani hii ni njama tuungane tushindwe kuendesha kampuni migodi iuzwe kwa wawekezaji,” anasema John Mika.

Wachimbaji wadogo wao, ushauri mkubwa wanaotoa kwa Serikali ni kufuata mapendekezo ya Tume ya Jaji Mark Bomani na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Generali Robert Mboma ya Mei 2002 kuwa madini ya Tanzanite yachimbwe na wachimbaji wadogo pekee kwa kuwa hayana ushindani katika soko la kimataifa.

Tume hiyo Mboma pia ilipendekeza itatue tatizo la mipaka baina ya kitalu B na C na kurejesha wa mwanzo wa mwaka 1987 na Serikali isitiwe leseni katika eneo la kitalu C kwa mwekezaji mkubwa na iwawezeshe wachimbaji wadogo kuchimba madini hayo.

Nini kitatokea sasa ili kumaliza mvutano huu unaowaondoa wazawa kuchimba madini, tusubiri kwani jambo hili linatarajiwa kuwa ajenda kubwa kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao Mkoa wa Manyara na Arusha.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment