Thursday 30 October 2014

WACHIMBAJI WALIA NA TANZANITEONE


Wachimbaji wadogo wa madini ya tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro wameishtaki kampuni ya TanzaniteOne kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wakidai kuwa imevamia na kupora baadhi ya migodi na zana za kufanyia kazi na kuharibu miundombinu yake.
 
Wakizungumza juzi na kamati hiyo iliyotembelea na kushuhudia baadhi ya migodi iliyoko Kitalu B (Opec), wachimbaji hao walidai kuwa wafanyakazi wa TanzaniteOne waliwavamia na kudai kuwa wanachimba kwenye eneo lao.

Meneja wa mgodi wa Deo Minja uliopo Opec, Omary Mandari alisema Septemba 8, mwaka huu, walivamiwa na watu hao waliopora tochi 38, nyaya za mita 1,000, diga tatu, huli 300 na wakakata mipira ya kupitisha upepo yenye mita 600.

“Tunadiriki kusema kampuni iliidharau kamati hii. Mlitoa agizo kuwa suala hili lisitishwe mpaka hapo mtakapotembelea eneo hili, tunashangaa hawakutekeleza badalika yake wakaamua kutuvamia na kufanya ukatili na uharibifu,” alisema Mandari.

Mmoja wa wamiliki wa mgodi katika eneo hilo, Mohamed Karia alidai kuwa walinzi wa kampuni hiyo waliingia mgodini kwake na kupora mashine mbili za kuchorongea na kuwajeruhi wafanyakazi wake kwa kuwapiga.

Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alisema mgogoro wa wachimbaji hao na TanzaniteOne unatokana na eneo hilo kugawanywa kisiasa, kwani wachimbaji hao ni wengi lakini wamepewa eneo dogo la mita 50 kwa 50.

“Wachimbaji wadogo walianza kuchimba tangu miaka ya 90. Mwaka 2004 wakaambiwa kuna sheria ilishatungwa na kutakiwa kila mmoja achimbe kwenye eneo lake, ndiyo ukawa mwanzo wa tatizo,” alisema Ole Sendeka.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Victor Mwambalaswa alisema watashughulikia tatizo hilo.la wachimbaji hao ambao wamekuwa wakilalamikia kila wanapokutana na viongozi wao wanapowafuata Bungeni mjini Dodoma.

“Kwa sababu tumeshuhudia tatizo hili hapa mgodini kesho (jana) tutakutana na viongozi wa wachimbaji wadogo wa Marema ili kutoa uamuzi wetu sisi kama Kamati ya Bunge kuhusu tatizo hili ambalo ni la muda mrefu sasa,” alisema Mwambalaswa.

Hata hivyo, Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya TanzaniteOne, Halfan Hayeshi alisema walinzi wa kampuni hiyo hawajawahi kuingia kwenye mgodi wowote wa mchimbaji mdogo na kufanya tukio lolote lile la kiuhalifu.

“Sisi tunafanya kazi kwenye maeneo yaliyopo katika kitalu chetu cha C ila hizo habari za kudai kwamba tumeingia eneo la migodi ya wachimbaji wadogo siyo za kweli, hatuwezi kufanya kitendo kama hicho,” alisema Hayeshi.

No comments:

Post a Comment