Sunday, 31 August 2014

MIRERANI

Uwekezaji ulivyoua Mji wa Mirerani

 
Kulia ni kibanda cha biashara kilichotelekezwa katika eneo la migodi ya Mirerani. Picha zote na Mussa Juma. 
 
Na Mussa Juma, Mwananchi
Kwa ufupi

Mirerani, Mji wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara ni moja ya miji iliyokuwa na umaarufu mkubwa, miaka 15 iliyopita kutokana na kuvutia maelfu ya watu, kutoka maeneo mbali mbali nchini


Mamia wahama, nyumba zabaki magofu, viongozi wa dini walia kukosekana sadaka na robo tatu ya migodi ya wachimbaji wadogo yafungwa.

Mirerani, Mji wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara ni moja ya miji iliyokuwa na umaarufu mkubwa, miaka 15 iliyopita kutokana na kuvutia maelfu ya watu, kutoka maeneo mbali mbali nchini.

Watu kutoka kila kona ya nchi na nje ya nchi walifika Mirerani kuchimba madini ya Tanzanite wengine kununua, wengi walinufaika kutokana na madini hayo na hivyo kuufanya mji wa Mirerani kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi.

Wakati huo, kila biashara halali na isiyo halali ilifanyika Mirerani, mji ulijengwa kila kona na msongamano wa watu ulikuwa mkubwa.

Sasa ukifika Mirerani hutaamini ndiyo ule mji uliokuwa na umaarufu mkubwa na kuvuta maelfu ya watu.

Ukiingia utapokelewa na magofu ya nyumba, maduka yaliyofungwa na watu wachache mitaani wengi wakiwa ni wazawa wa mji huo.

Wengi waliokwenda Mirerani, kufuata tanzanite wamehama na wengine walibomoa nyumba zao na kuuza mabati ili kupata nauli ya kurejea makwao.

Majumba ya starehe na migahawa ambayo iliikuwa ikifurika watu, sasa hakuna watu na baadhi wamebadili matumizi.

Hali hii haipo katika mji wa Mirerani tu, bali hata maeneo ya migodi ya kitalu B maarufu kama OPEC na D ambavyo humilikiwa na wachimbaji wadogo, wachimbaji wadogo sasa ni wachache sana tofauti na miaka ya nyuma.

Katika machimbo haya sasa ukifika utakutana na wachimbaji wachache waliochoka na wengine wakiwa wamelala pembezoni mwa barabara zilizochakaa.

Mamia ya vijana waliokuwa wanategemea uchekechaji wa mchanga maarufu kama wanaapolo pembezoni mwa migodi ili wapate tanzanite sasa hawapo tena, kwani hakuna kinachopatikana katika maeneo ya wachimbaji wadogo.
Nini kimeikumba Mirerani 

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi na kuthibitishwa na viongozi wa serikali, viongozi wa dini na wachimbaji wadogo, umebaini kuwa chanzo cha cha kuzorota uchumi wa Mirerani ni wananchi wengi kutegemea madini ya Tanzanite ambayo sasa hawapati.
Madini sasa kwa kiasi kikubwa yanapatikana katika eneo la kitalu C ambacho kinamilikiwa na mwekezaji kampuni ya Tanzanite One na sheria ya madini imezuia wachimbaji wadogo kugusa eneo la mwekezaji.

Justine Nyari ni Diwani wa Mirerani anasema maisha magumu ya Mirerani yamesababishwa na mwekezaji kwani hana faida kwa wananachi.

Anasema asingekuwepo mwekezaji wananchi wangeendelea kuchimba madini hadi sasa hata kama wangekuwa wanapata kidogo kidogo, lakini maisha yao yangekuwa bora kama zamani.

“Mji wa Mirerani maisha ni magumu sana kwa sasa, watu hawana fedha na wengi wamehama na Tanzania ukitaka kuona athari za uwekezaji njoo Mirerani,” alisema Nyari.

Kaimu Mtendaji wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Raphael Chao anasema kuzorota kwa shughuli nyingi Mirerani, kumesababishwa na wananchi kutegemea madini ya Tanzanite.

Anasema wachimbaji wadogo ndiyo, walikuwa wadau wakuu wa maendeleo Mirerani ambao sasa hawapati tena madini kama zamani.

Alisema ingawa eneo hilo, kuna Mwekezaji kampuni ya Tanzanite One, lakini mamlaka ya mji mdogo Mirerani hawanufaiki ipasavyo.

“Wachimbaji wadogo wanapopata madini mji unachangamka na mabadiliko yanaonekana kwani wachimbaji wengi ni wenyeji wa hapa hivyo, wafanyabiashara watanufaika na hata shughuli nyingine zitanufaika,” anasema.

Anafafanua kuwa kwa mwekezaji akipata madini, yeye analipa kodi serikali kuu, Mji wa Mirerani haunufaiki moja kwa moja kwani hakuna kodi inayolipwa Mirerani, “anasema.

Sadiki Mnenei ni Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo mkoa wa Manyara (MAREMA), anasema bila jitihada maalumu, mji wa Mirerani utakufa kwani wananchi wengi wanategemea madini ya Tanzanite ambayo sasa yamehodhiwa na mwekezaji kampuni ya Tanzanite One.

Mnenei anasema miaka 15 iliyopita wachimbaji wadogo walikuwa na uwezo, kwani walikuwa wanapata madini na kuuza na walikuwa wanatoa ajira zaidi ya vijana 10,000.

Anasema sasa migodi mingi imesimama kutokana na gharama kubwa za uchimbaji kutokana na madini kupatikana mbali na pia hata zana za uchimbaji zimekuwa ghali.

“Tulikuwa tunanunua baruti Sh120, 000 hadi 140, 000 kwa katoni lakini sada ni zaidi ya Sh 200, 000 hadi 250, 000 bado bei za mafuta zipo juu na sheria mpya ya madini inatubana sana,” anasema.

Anasema sasa migodi ya wachimaji wadogo, madini yapo mbali na sehemu ambayo madini yanapatikana ni eneo kubwa alilopewa mwekezaji na kulingana na sheria ya madini iliyopitishwa inakataza kuchimba kufuata miamba ya madini.

“Sisi wenyewe tuna sheria zetu za uchimbaji kwa kuwa madini haya hayachimbwi kama choo kwa kwenda chini tu, tuna kamati za usuluhishi kama mchimbaji mmoja ameingia eneo la mwingine basi anarudi nyuma kufuata njia nyingine”anasema

Lakini anasema kwa sasa miamba yote ya madini inaelekea kitalu C kinachomilikiwa na Tanzanite One hivyo kuzuiwa kuchimba chini ya ardhi ni kutuondoa wachimbaji wadogo Mirerani.

Anasema wachimbaji wadogo ndio walikuwa nguzo ya maendeleo Mirerani, kwani ndio walichangia ujenzi wa zahanati,Kituo cha polisi Mirerani na kivuta umeme migodini na Mirerani.
Anasema hata biashara ya madini, imehodhiwa na mwekezaji kwani ana madini mengi na hivyo, soko la madini anaweza kuliyumbisha jambo ambalo linawaathiri wachimbaji wadogo.
Viongozi wa dini nao walia kusimama miradi. 
Viongozi wa dini katika mji wa Mirerani, wanaeleza kilio Chao cha kuzorota shughuli mbali mbali katika nyumba za ibada kutokana na wananchi wengi kutegemea madini ya tanxanite ambayo sasa hawapati.
Sheikh Idd Mohamed ni imamu wa msikiti mkubwa wa Mirerani Musjid Noor, anasema hali ya Mirerani siyo nzuri na lazima serikali ichukuee hatua kuukomboa mji huo.

No comments:

Post a Comment