Friday 29 November 2013

WANACHAMA WATATU MAMEC WAFUKUZWA




Waandishi watatu wa Klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara, Mamec, wamevuliwa uanachama wao kutokana na kukosa maadili baada ya kufunga kwa kufuli ofisi ya klabu hiyo.

Uamuzi huo mgumu ulichukuliwa mjini Babati na wanachama wa Mamec baada ya kusomewa na Mwenyekiti wao Benny Mwaipaja uamuzi wa kamati ya maadili iliyopendekeza wachukuliwa hatua baada ya wao kugoma kufika.

Wanachama hao waliwafutia uanachama waandishi hao ambao ni Charles Masayanyika wa kituo cha ITV na Radio One, Hamida Khalid wa gazeti la Tanzania Daima na na Tabia Daffo wa Radio Uhuru.   

Ilidaiwa kuwa, wanachama hao watatu walifunga ofisi ya Mamec, Novemba mosi mwaka huu wakidai kuwa hawautambui uongozi uliopo hivyo uamuzi uliotolewa ni kuwafutia uanachama kutokana na kukosa maadili
“Waandishi hawa waliitwa kwenye kamati ya Maadili, Usuluhishi na Nidhamu lakini wakagoma kufika hivyo kamati hiyo ikapendekeza wapewe onyo au adhabu ambayo wanachama wanaona inafaa,” alisema Bw Mwaipaja.

Pia, wanachama hao walikubali kwa ridhaa yao kujiuzulu kwa Katibu Mtendaji wa Mamec, Zacharia Mtigandi wa Star TV, aliyeandika barua ya kujiuzulu ambapo nafasi yake itashikiliwa na Abraham Mlundi wa gazeti la Ohayoda.

Pamoja na hilo wanachama hao waliridhia kujiuzulu kwa mjumbe wa kamati tendaji, Hamida Khalidi ambapo nafasi yake ilijazwa na Joseph Simba wa gazeti la Ohayoda.

Makamu Mwenyekiti wa Mamec, Mary Margwe alisema hatua hiyo ya kuwafukuza uanachama waandishi hao imechukuliwa ili kuleta nidhamu kwenye chama na watachukua hatua kali endapo hali hiyo itajitokeza tena.

“Bora tubaki wanachama wawili wenye malengo ya 
kutumikia jamii kwa ufasaha kuliko kuwa na kundi kubwa la wanachama, sisi tupo 17 tu lakini tunaanza kufunga ofisi badala ya kuleta hoja mezani,” alisema Margwe.

Hata hivyo, wanachama wa Mamec, wamepongeza hatua hiyo ya kufukuzwa uanachama waandishi hao watatu kwani ni muda mrefu walikuwa wanasababisha fujo zenye lengo la kuanzisha migogoro.

No comments:

Post a Comment