Saturday, 20 May 2017

DC MBULU AWAASA WANANCHIMkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amewataka wakazi wa Kijiji cha Guye kuacha malumbano na kujenga madarasa ya shule ya msingi kwa muda wa mwezi mmoja.

Mofuga akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, alisema anahitaji apatiwe mpango wa maendeleo wa kijiji, apatiwe taarifa hiyo ofisini kwake ikiwemo kujenga madarasa kwa mwezi mmoja.

Alisema pamoja na serikali kuwa na sera ya elimu bure na elimu bila malipo lakini wananchi wanapaswa kujenga madarasa ya shule ili wanafunzi wao waweze kupata elimu kwenye mazingira mazuri.

“Ni kijiji cha ajabu kweli kweli, yaani ninyi mnakaa mwaka mzima lakini hakuna shughuli za maendeleo, kule watoto wanasoma wenu wanasoma kwa mazingira magumu ya madarasa,” alisema Mofuga.

Alisema endapo kuna mapungufu mengine kwenye shule hiyo ikiwemo nyumba za walimu, wananchi hao wanapaswa kuhakikisha yanajengwa kwani hiyo ni kwa jaili ya faida ya watoto wao.

Mkazi wa kijiji hicho cha Guye, John Akonaay alisema anasikitishwa na kitendo cha baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kuwa na mwamko mdogo wa kuchangia kutokana na ufujaji wa fedha uliofanyika.

“Tunashukuru mkuu wa wilaya leo (juzi) umeagiza yule mtendaji wa kijiji aliyefuja fedha zetu amekuja na kujibu tuhuma kuwa atazilipa ila tukichanga tena huyu mtendaji mpya asizifuje,” alisema Akonaay.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Adam Sule alisema anasikitishwa na kitendo cha kuambiwa kuwa wakili aliyekuwa anafuatilia kesi ya ufujaji wa fedha za kijiji anawadai sh1.5 milioni hivyo walipe.

“Tulishamlipa huyo mwanasheria lakini hivi sasa bado tunaambiwa tunadaiwa ili hali kwenye taarifa ya awali inaonyesha alishalipwa sh150,000 ya usafiri wa kutoka Babati hadi hapa,”  alisema Sule.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment