Friday 7 April 2017

WATAKIWA KUWAUNGA MKONO WAWEKEZAJI



Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Sipitieck amewataka wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani kuwapa ushirikiano wawekezaji wa TanzaniteOne na siyo kuwabeza.

Sipitieck amesema wananchi wa mji mdogo wa Mirerani wanapaswa kuwa wazalendo kwa kuwaunga mkono na kushirikiana na wawekezaji wa kampuni ya TanzaniteOne kuliko kuwavunja moyo.


Aliyasema hayo juzi wakati akiushukuru uongozi wa kampuni ya TanzaniteOne waliotoa ahadi ya msaada wa kujenga madarasa saba ya shule ya msingi Songambele ambayo madarasa yake yaliharibika.

Alisema baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamekuwa na kigeugeu kwani wakati mwingine kuwabeza wawekezaji hao na siku inayofuata huisifu TanzaniteOne, hivyo wawe na msimamo mmoja unaoeleweka.

“Nadhani ifike mwisho kwa wananchi kuwabeza wawekezaji ambao hutumia nafasi yao kwa kusaidia jamii katika baadhi ya miradi, kupitia kile wanachokipata kwenye uwekezaji huo,” alisema Sipitieck.

Alisema awali halmashauri hiyo ilitaka kuhamisha shule hiyo ambayo tangu mwaka 2013 iliharibika baada ya kupitiwa na mafuriko makubwa ila kampuni hiyo imeahidi kuijenga upya kwa ubora zaidi.




Mkurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne Faisal Shabhai alisema ana imani kubwa kuwa wataendelea kushirikiana jamii ya eneo hilo na kampuni hiyo katika kuhakikisha wanawezesha miradi ya jamii.

“Hivi sasa tunafungua ukurasa mpya kwa kushirikiana nanyi kama kawaida kwa kuhakikisha kile kidogo tunachokipata tunakigawa kwa jamii inayozunguka sehemu ya uwekezaji wetu,” alisema Shabhai.

Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Adamu Kobelo alisema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kuweka kipaumbele kwenye miradi ya jamii na siyo mtu mmoja mmoja kupewa fedha.

Mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo, Japhary Matimbwa alisema anaishukuru kampuni ya TanzaniteOne kwa kusaidia baadhi ya miradi ikiwemo kuichimbia kisima shule ya awali na msingi Kazamoyo.


“Wapo watu ambao kipindi cha uwekezaji wa mzungu walikuwa wanapiga bomu na kujinufaisha wenyewe ila sasa hivi wamekuja wawekezaji wazuri ila wachache wanapinga,” alisema Matimbwa.

No comments:

Post a Comment