Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
Mkoa wa Manyara, umekabidhi mashuka 170 kwenye zahanati ya Kijiji cha Engusero
na hospitali ya wilaya ya Kiteto kwa ajili ya kutumiwa kujifunika na wagonjwa
wanaofika kulazwa.
Mashuka hayo yalikabidhiwa kwa mkuu wa
wilaya hiyo Kanali Samuel Nzoka na meneja wa NHIF wa mkoa huo Isaya Shekifu,
kwenye uzinduzi wa uhamasishaji wa kujiunga mfuko wa afya ya jamii (CHF)
uliofanyika kwenye kijiji cha Engusero.
Akizungumza wakati akipokea mashuka
hayo Kanali Nzoka aliushukuru mfuko huo na kuzitaka kaya za eneo hilo kujiunga
na CHF ili wajipatie matibabu kwa mwaka mzima kwani kaya moja yenye watu sita
italipia sh10,000.
Alisema tatizo la
ukosefu wa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitalini litamalizika,
endapo kaya nyingi zikijiunga na CHF kwani serikali nayo itaweka mkono wake ili
kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa.
Wakati wa uzinduzi wa
zoezi hilo Kanali Nzoka alijitolea sh20,000 kwa ajili ya kuzilipia kaya mbili
za watu 12 wa kijiji cha Engusero na Dosidosi na kuungwa mkono na viongozi
wanne wa wilaya hiyo waliojitolea sh10,000 kwa kila mmoja.
Kwa upande wake,
Shekifu alisema mwanachama wa CHF atanufaika na huduma zote za afya za msingi
za kinga na tiba zitolewazo katika zahanati, kituo cha afya na hospitali
ikiwemo huduma za wagonjwa wa kutwa na kulazwa.
Alitaja huduma
nyingine ambazo zitatolewa kwa mwaka mmoja kwa kuchangia sh10,000 ni vipimo vya
maabara, upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na halmashauri husika na
wanachama kupata huduma bora ya afya.
“Pia watapata huduma
ya upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na Halmashauri zinazoendesha
mifuko hii zinapata mapato ya tele kwa tele kutoka serikalini ambayo yatatumika
kuboresha huduma za afya,” alisema.
Ofisa uratibu na
matokeo wa CHF, Nicholaus Mwangomo alisema mpango huo ulianzishwa kwa sheria
namba moja ya mwaka 2001 sura ya 409 ya sheria ya Tanzania toleo la 2002 wa
kaya au familia kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua.
Mwangomo alisema
sababu za kuanzishwa CHF ni kuiwezesha jamii kumiliki huduma za afya
zinazowahusu katika maeneo wanayoishi, kuchangia huduma za afya kwa wananchi na
kuboresha huduma za matibabu kwa utaratibu rahisi.
No comments:
Post a Comment