Joseph
Lyimo,Mirerani
NAIBU
Waziri wa Nishati na Madini,Stephen Masele ameiamuru kampuni ya TanzaniteOne
kuacha kumwaga maji kwenye migodi ya wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite
wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Akizungumza na uongozi wa kampuni hiyo,Masele ambaye ni Naibu Waziri anayeshughulikia
madini aligeuka na kuwa mkali mithili ya mbogo wakati akizungumzia suala hilo
kwa viongozi wa kampuni hiyo.
Naibu
waziri alitoa amri hiyo baada ya kuelezwa na wachimbaji wadogo alipofanya ziara
ya kutembelea migodi yao kuwa kampuni hiyo inawamwagia maji mgodini na alipotoa
amri hiyo gari lake lilisukumwa na wachimbaji hao.
“Sawa
hawa ni wawekezaji lakini Serikali haipo tayari kuona wachimbaji wadogo
wananyanyaswa katika nchi yao hivyo nimeiamuru kampuni hiyo kusitisha mara moja
kumwaga maji hayo,” alisema Masele.
Hata
hivyo,Mwenyekiti wa kampuni ya TanzaniteOne,Ammi Mpungwe alimthibitishia Masele
kuwa kampuni yake haimwagi maji kwenye migodi ya wachimbaji wadogo ila maji hayo
yanatoka yenyewe kwenye mgodi wa TanzaniteOne.
Mpungwe
alisema maji hayo hutoka nyenyewe kutokana na jiolojia ya miamba ilivyo kwenye
mgodi wao wa Bravo ambao haufanyiwi kazi lakini kampuni hiyo haijawahi kumwaga
maji kwenye migodi ya wachimbaji wadogo.
“Mheshimiwa
waziri mimi nilikuwa balozi na nikastaafu kwa heshima zote,sasa siwezi kwenda
jela leo kwa kosa la kukiuka sheria za nchi,mimi ni mzalendo sitakubali
kuruhusu kampuni yetu imwage maji migodini,” alisema Mpungwe.
Pia,Naibu
Waziri huyo aliitaka kampuni hiyo kusaidia huduma za jamii kama madawati
shuleni,afya na maji kwenye kata zote nne za tarafa ya Moipo wilayani humo
kuliko kuisaidia kata moja ya Naisinyai.
“Watanzania
hawatatuelewa ikiwa kampuni hii inachimba madini ya Tanzanite yenye utajiri
mkubwa wakati kata za jirani wanafunzi wanakaa sakafuni,huduma za afya duni na barabara ya
Kia-Mirerani ni ya vumbi,” alisema Masele.
Akizungumzia
kuhusu hilo,Mpungwe alisema watajipanga kulitekeleza ila alisikitishwa na
kitendo cha viongozi wa kilichokuwa kijiji cha Mirerani kukataa msaada wa zaidi
ya sh12 milioni walizotoa kama msaada wa maendeleo mwaka 2000.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment