Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, limepitisha shilingi bilioni 43.983 za
mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga, akizungumza baada ya kupitishwa bajeti hiyo,
alisema vipaumbele vyake ni elimu, afya, maji, kilimo na mifugo.
Kamoga alisema bajeti hiyo
imezingatia vipaumbele vya vijiji, kata, halmashauri, mkoa, mpango wa pili wa
maendeleo ya Taifa na dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.
Alisema vipaumbele vingine ni
mikakati na sera mbalimbali za kisekta, maelekezo mbalimbali ya viongozi wakuu
wa kitaifa, na ahadi ya Rais John Magufuli alizozitoa wakati wa kampeni
wilayani Mbulu.
Alisema halmashauri hiyo imejikita
katika kuongeza mapato ya ndani kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo, kubuni vyanzo
vipya na kuimarisha mfumo wa kielectroniki.
"Halmashauri imejikita katika
mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa makazi, biashara, viwanda vidogo, maeneo
ya malisho ya mifugo, kilimo, hifadhi ya mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya
maji," alisema Kamoga.
Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini,
Flatei Massay alipongeza kupitishwa kwa bajeti hiyo ambayo imekidhi kuondoa
changamoto mbalimbali.
Massay alisema bajeti hiyo imegusa
sekta mbalimbali ikiwemo elimu ya msingi, sekondari, kilimo, mifugo, ushirika,
umwagiliaji, afya na maji.
Alisema anatarajia wananchi wa jimbo
hilo watapiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya mpango
wa bajeti iliyopishwa na madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Mwanasheria wa halmashauri hiyo,
Honoratus Mulokozi alisema bajeti hiyo kabla ya kupitishwa imezingatia sheria
namba 9 ya serikali za mitaa ya mwaka 1982.
Mulokozi alisema sheria hiyo ilifanyiwa
marekebisho Januari mosi mwaka 2000 inayotaka kufuata sheria, kanuni na
taratibu, wakati wa kuandaa bajeti.
No comments:
Post a Comment