Wachimbaji wadogo wa madini, wachuuzi na
madalali wa madini nchini wanatarajia kufanya mdahalo wa kitaifa juu ya umuhimu
wa sekta ya madini na namna ya kuwanufaisha zaidi.
Mkurugenzi wa shirika la Haki Madini Amani
Mhinda, akizungumza mji mdogo wa Mirerani na viongozi wa chama cha
wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema) alisema mdahalo huo utafanyika mkoani
Geita.
Mhinda alisema lengo la mdahalo huo ni
kuwaleta wadau mbalimbali kwa pamoja ili kuzungumzia changamoto zinazoikabili
sekta hiyo kwa wachimbaji wadogo na kutafakari kitaifa maono ya wachimbaji.
Alisema wanatarajia kufanya mdahalo huo
mwishoni mwa mwezi Juni kwa kushirikiana na shirika kiongozi duniani la
maendeleo la International Institute for Environment and Development (IIED).
“Haki madini tunarajia mpango huu utatoa jukwa
hitajika kwa wadau kushirikiana na kubadilishana ujuzi na kukuza utawala bora
kuwa sauti kubwa, usalama na utengenezaji,” alisema Mhinda.
Alisema uchimbaji mdogo wa madini unaweza
kutoa mchango chanya wenye umoja na usawa wa maendeleo endelevu na ukuaji wa
uchumi, kwani husaidia mamilioni ya watu hasa wanawake na watoto.
Katibu wa Marema Tawi la Mirerani, Abubakari
Madiwa alisema kupitia mdahalo huo wanatarajia wachimbaji mdogo kunufaika kwa
kujengewa uwezo hivyo wamejiandaa kushiriki mara utakapofanyika.
“Haki madini imekuwa msaada mkubwa kwa
wachimbaji madini wadogo kwani tumekuwa pamoja bega kwa bega kwa kuhakikisha
wachimbaji wadogo wanapata haki zao,” alisema Madiwa.