Saturday, 28 May 2016

SIMANJIRO WAASWA KUTUMIA MBOLEA



Wakulima wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kubadilika kwa kulima kitaalamu ikiwemo kutumia mbegu bora na mbolea za kupandia na kukuzia ili kuondokana na dhana potofu kuwa mbolea inafubaza ardhi.

Ofisa kilimo na umwagiliaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Claudy Losiock akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya Mahmoud Kambona na madiwani waliofika shambani kwake, alisema ameamua kuandaa shamba hilo ili atoe somo.

Losiock alisema kupitia shamba darasa hilo la kwake viongozi na wananchi watajifunza na kuwaelimisha wakulima wengine faida ya kulima kitaalamu kwa kutumia mbegu bora, mbolea za kupandia na kukuzia.

Alisema kwa sababu ya taaluma yake ameandaa shamba lake lenye ukubwa wa ekari nne na akalima zao la mahindi kwa ajili ya mafunzo kwa wakulima wa eneo hilo ili wafahamu faida ya kulima na kutumia mbolea na mbegu bora.   



Akizungumza kwenye shamba hilo, mkuu wa wilaya hiyo Kambona alisema ni vizuri viongozi wa kisiasa wenye ushawishi mkubwa kwa jamii za kifugaji kupata somo hilo la kilimo bora ili wakatoe elimu kwa wapiga kura wao nao waige.

“Dhana potofu ya kuwa mbolea zinaharibu ardhi hivi sasa zimepitwa na wakati kwani wakulima bora hulima kitaalamu kwa kuwatumia maofisa ugani wanaowaelimisha na kupata mazao mengi na yenye tija,” alisema Kambona.

Diwani wa kata ya Terrati Jackson Ole Materi, alisema kupitia shamba darasa la Losiock, naye amepata somo zuri kwa ajili ya kuwaeleza wakulima wa eneo lake na yeye atatumia shamba lake kwa ajili ya kulima mahindi kitaalamu zaidi.

“Kazi ya kilimo ni nzuri na endapo utafuata vigezo utafanikiwa kupata mazao bora kwani kuna baadhi ya watu wanalima kwa mazoea ekari 20 na kupata mavuno sawa sawa na yule aliyelima ekari 10 kitaalamu,” alisema Ole Materi.



Diwani wa kata ya Naberera Haiyo Mamasita, alisema atawachukua baadhi ya wakulima wa eneo lake kwa ajili ya kufika kaya ya Orkesumet lilipo shamba hilo ili wajionee ubora ulivyo na kupata funzo ya shamba darasa hilo la ofisa kilimo.

“Tumezoea kuona baadhi ya watu wanakuwa na taaluma fulani lakini hawana matokeo mazuri kwenye uhalisia, kwani kuna mafundi seremala hawana hata stuli lakini huyu ofisa kilimo ana shamba darasa zuri,” alisema Mamasita.

No comments:

Post a Comment