Mbunge wa Jimbo la
Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya amesema ataanzisha kamati ya wadau
wa maendeleo ya Simanjiro, itakayoongozwa na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Singida
Parseko Kone.
Ole
Millya alisema hawezi kuwaweka kando wasomi wa wilaya hiyo, hivyo atawakumbatia
kwani Simanjiro haiwezi kuendelea bila ushirikiano wa wadau mbalimbali wenye
maono ya kuifikisha mbali.
Alisema ameshapata msaidizi
wake, Joshua Kuney ambaye ni katibu wa mbunge hivyo kilichobakia ni kuhakikisha
timu hiyo inakutana mara moja kwa kushirikiana na wazee wa mila watafanikisha
maendeleo.
Diwani wa kata ya Naberera
Haiyo Mamasita, alisema hivi sasa uchaguzi umeshapita hivyo kinachotakiwa ni
kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanapatikana ikiwemo huduma muhimu za kijamii
za maji, elimu na afya.
“Changamoto kubwa iliyopo
hivi sasa ni kuhakikisha suala zima la elimu linafanikiwa kwenye kata yetu ya
Naberera na nitahakikisha wanafunzi waliokuwa wanakosa hiyo fursa
wanafanikiwa,” alisema Mamasita.
Ole Millya alisema miongoni mwa wadau
wa maendeleo na wasomi watakaokuwa kwenye kamati hiyo ambayo haitajadi itikadi
za kisiasa ni mkuu wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Peter Toima na Katibu wa
Chadema Simanjiro Frank Oleleshwa.
“Siwezi kuwakataa wasomi wa
Simanjiro kwani tutashirikiana nao tupate maendeleo, nataka mwisho wa siku
ikifika uchaguzi kama kunipa mnipe ninyi wenyewe na kama kuninyima mninyime
wenyewe,” alisema Ole Millya.
Alisema huwezi kufanikiwa
maendeleo ya wananchi wa Simanjiro ili hali unaogopa kushirikiana na wasomi,
kwani japokuwa wengine wapo nje ya eneo hilo lakini kupitia ushirikiano
waliouanzisha watafanikisha mambo mengi.
No comments:
Post a Comment