Monday, 4 April 2016

WACHIMBAJI WAANDAMANA


Wachimbaji 70 wadogo (WanaApolo) madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa kampuni ya G and M, wameandamana wakipinga kufukuzwa kazi bila kulipwa madai yao.

Wachimbaji hao wanyonge wanadai kuwa walifanya kazi kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu kwenye mgodi huo, ambao unafanya shughuli zake kwa ubia na kampuni ya wachina, lakini wamefukuzwa mgodini huku wakinyimwa stahiki zao.

Wakizungumza nje ya mgodi huo, wanyonge hao walidai kuwa wamefanya kazi kwa muda wote huo ikiwemo kuanzisha mgodi na kujenga ukuta wa matofali ya saruji bila kulipwa fedha zao.


Mmoja kati ya wachimbaji hao Jonas Mgendi alisema baada ya kutumia nguvu za kuchimba kwenye mgodi huo walichokipata ni kufukuzwa kazi bila kulipwa chochote hivyo serikali inapaswa kuingilia kati ili wapate haki yao.

Mchimbaji mwingine Joseph William alisema kampuni hiyo na hao wachina, wametumia nguzu zao bure bila kuwapa haki zao na kila mtu anayeonekana adai fedha anaandikwa jina na kufukuzwa ili wawachukue wafanyakazi wapya.

“Tunaiomba serikali iwachukulie hatua hii kampuni pamoja na wachina wao kwani sisi tumefanya kazi kwa zaidi ya muda wa miaka mitatu mfululizo lakini tulichoambulia ni kufukuzwa kazi huku mafao yetu tukikosa,” alisema William.

Hata hivyo, meneja wa mgodi huo Elisante Forget alisema wachimbaji hao walikuwa vibarua wao na siyo wafanyakazi wa kampuni yao ya G and M mining Co Ltd, kwani hawana mkataba nao wowote wa kuwapa ajira.

Forget alisema waliandika barua Wizara ya Nishati na Madini ya Desemba 29 mwaka jana ya kusimamisha shughuli zote za uendeshaji wa mgodi kutokana na kampuni kukosa fedha za kufanyia kazi hadi hapo watakapopata fedha.  

“Hao wanaodai walikuwa wafanyakazi wetu hatuwatambui na hawatudai fedha zozote, kwani sisi baada ya kuanza tena shughuli zetu, tulitangaza nafasi za vibarua wapya na ndiyo hawa ambao wanafanya kazi hivi sasa,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa soko la kitalu D John Njau alisema mara nyingi wamiliki wa migodi huwaeleza wafanyakazi wao kuwa hawana uwezo wa kuwapa fedha zaidi ya huduma za chakula, malazi na matibabu pindi wakiugua.

No comments:

Post a Comment