Saturday 10 August 2013

WACHIMBAJI TANZANITE WAOMBA MIGODI IFUNGULIWE



Wachimbaji madini wa migodi minne ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ambayo imesimamishwa kufanya kazi wameiomba Serikali kuifungulia, ili waendelee na shughuli zao za uchimbaji.

Wachimbaji hao waliogoma kutaja majina yao walisema tangu wasimamishwe kazi Julai 23 mwaka huu, baada ya mchimbaji wa TanzaniteOne kuuawa kwa kupigwa risasi na mtu asiyejulikana, haijakaguliwa kama Serikali ilivyoagiza.

Wachimbaji hao walisema migodi hiyo yenye kutoa ajira kwa wachimbaji zaidi ya 2,000 mbali na familia zao, hivi sasa wameathirika kwani wanaishi bila kufanya kazi, hivyo wanapata wakati mgumu kupata fedha za kujikimu.

Pia walisikitishwa na kitendo cha migodi yao kusimamishwa kazi, huku migodi ya kampuni ya TanzaniteOne wanayopakana nayo ikiendelea kufanya kazi na kuwapa mshangao kwa kukosekana usawa katika uchimbaji madini.




“Tunaomba Serikali ifanye uchunguzi wao kwa haraka na busara ili sisi tuweze kuendelea na kazi zetu, kwani hata Joseph Mwakipesile Chusa wamemshikilia kwa shinikizo tu la wachimbaji wa kampuni hiyo, hausiki na lolote,” walisema.

Walidai kuwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo huwa wanashirikiana na wachimbaji wasio rasmi katika kufanya kazi kwenye kampuni hiyo na pindi wakidhulumiana ndiyo hutokea matatizo na kusingizia wachimbaji wadogo.

Hata hivyo, Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Abubakary Madiwa alikiri kupata barua  ya wachimbaji hao kulalamika kufungiwa migodi hiyo kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment