Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Sipitieck amewataka wakazi wa Mji mdogo wa
Mirerani kuwapa ushirikiano wawekezaji wa TanzaniteOne na siyo kuwabeza.
Sipitieck amesema wananchi wa mji mdogo wa
Mirerani wanapaswa kuwa wazalendo kwa kuwaunga mkono na kushirikiana na
wawekezaji wa kampuni ya TanzaniteOne kuliko kuwavunja moyo.
Aliyasema hayo juzi wakati akiushukuru uongozi
wa kampuni ya TanzaniteOne waliotoa ahadi ya msaada wa kujenga madarasa saba ya
shule ya msingi Songambele ambayo madarasa yake yaliharibika.
Alisema baadhi ya wananchi wa eneo hilo
wamekuwa na kigeugeu kwani wakati mwingine kuwabeza wawekezaji hao na siku
inayofuata huisifu TanzaniteOne, hivyo wawe na msimamo mmoja unaoeleweka.
“Nadhani ifike mwisho kwa wananchi kuwabeza
wawekezaji ambao hutumia nafasi yao kwa kusaidia jamii katika baadhi ya miradi,
kupitia kile wanachokipata kwenye uwekezaji huo,” alisema Sipitieck.
Alisema awali halmashauri hiyo ilitaka
kuhamisha shule hiyo ambayo tangu mwaka 2013 iliharibika baada ya kupitiwa na
mafuriko makubwa ila kampuni hiyo imeahidi kuijenga upya kwa ubora zaidi.
Mkurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne Faisal
Shabhai alisema ana imani kubwa kuwa wataendelea kushirikiana jamii ya eneo
hilo na kampuni hiyo katika kuhakikisha wanawezesha miradi ya jamii.
“Hivi sasa tunafungua ukurasa mpya kwa
kushirikiana nanyi kama kawaida kwa kuhakikisha kile kidogo tunachokipata
tunakigawa kwa jamii inayozunguka sehemu ya uwekezaji wetu,” alisema Shabhai.
Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani
Adamu Kobelo alisema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kuweka kipaumbele kwenye
miradi ya jamii na siyo mtu mmoja mmoja kupewa fedha.
Mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo, Japhary
Matimbwa alisema anaishukuru kampuni ya TanzaniteOne kwa kusaidia baadhi ya
miradi ikiwemo kuichimbia kisima shule ya awali na msingi Kazamoyo.
“Wapo watu ambao kipindi cha uwekezaji wa
mzungu walikuwa wanapiga bomu na kujinufaisha wenyewe ila sasa hivi wamekuja
wawekezaji wazuri ila wachache wanapinga,” alisema Matimbwa.