Mkuu wa
Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera amewataka viongozi wa Wilaya kuhakikisha
wanashirikiana ipasavyo ili kutatua migogoro ya ardhi inayorudisha nyuma
maendeleo kwani robo tatu ya mkoa huo imegubikwa na migogoro.
Dk Bendera
akizungumza mjini Babati kwenye mafunzo elekekezi kwa viongozi wa wilaya
za mkoa huo alisema, migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa ndiyo kikwazo cha
maendeleo hivyo watumie uwezo wao wote ili kuimaliza.
Alisema kila
kiongozi kwa nafasi yake anapaswa kuhakikisha anasimama vyema katika kutekeleza
majukumu zaidi kwani migogoro mingi inaweza kumalizika endapo itatiliwa maanani
kwenye utekelezaji ili kupiga hatua ya maendeleo.
Alisema migogoro
ya ardhi ambayo imetawala kwenye robo ya sehemu ya Manyara inapaswa kumalizika
kwa kuhakikisha viongozi wote wa wilaya wanawajibika kumaliza migogoro hiyo
isiyokuwa na faida yoyote.
“Tunapaswa
kutimiza wajibu wetu ipasavyo kwa kuhakikisha viongozi wa kisiasa na watendaji
wanatumia nafasi zao kikamilifu ili kumaliza migogoro hiyo ambayo haina manufaa
kwa wananchi tunaowaongoza,” alisema Dk Bendera.
Mkuu wa wilaya ya
Kiteto Tumaini Magessa, alisema matatizo mengi ya mkoa wa Manyara kuhusu
migogoro hiyo ni kutokuwepo kwa matumizi bora ya ardhi kwani wilaya hiyo
imetumia miaka 10 kusuluhisha migogoro na haijamalizika.
“Wilaya yetu imetumia
miaka mingi mno kwa ajili ya kusuluhisha migogoro ili hali tungeweza kutumia
muda huo kwa ajili ya kujenga madarasa, shule na kufanya maendeleo mengine
hivyo tunapaswa kubadilika,” alisema Magessa.
Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Yefred Mnyenzi alisema inapaswa
sheria, taratibu na kanuni (STK) zifuatwe katika utekelezaji kwani kuna baadhi
ya watu wanamilikishwa ardhi bila kufuata utaratibu halali.
Mkuu wa wilaya ya
Simanjiro Zephania Chaula alisema viongozi wa wilaya yake na wilaya ya Kiteto
watakutana hivi karibuni ili kusuluhisha mgogoro wa ardhi uliopo kwenye kata ya
Emboreet Simanjiro na kata ya Makame Kiteto.
Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Tamimu Kambona alisema wanakabiliwa
na migogoro mingi ya mipaka kwenye wilaya jirani ikiwemo Kilindi, Gairo, Chemba
na Simanjiro hivyo mkoa ushiriki kuitatua.