Wachimbaji
70 wadogo (WanaApolo) madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani
Manyara, waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa kampuni ya G and M, wameandamana
wakipinga kufukuzwa kazi bila kulipwa madai yao.
Wachimbaji
hao wanyonge wanadai kuwa walifanya kazi kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu kwenye mgodi
huo, ambao unafanya shughuli zake kwa ubia na kampuni ya wachina, lakini
wamefukuzwa mgodini huku wakinyimwa stahiki zao.
Wakizungumza nje ya mgodi huo, wanyonge hao walidai kuwa wamefanya kazi
kwa muda wote huo ikiwemo kuanzisha mgodi na kujenga ukuta wa matofali ya
saruji bila kulipwa fedha zao.
Mmoja
kati ya wachimbaji hao Jonas Mgendi alisema baada ya kutumia nguvu za kuchimba
kwenye mgodi huo walichokipata ni kufukuzwa kazi bila kulipwa chochote hivyo
serikali inapaswa kuingilia kati ili wapate haki yao.
Mchimbaji
mwingine Joseph William alisema kampuni hiyo na hao wachina, wametumia nguzu
zao bure bila kuwapa haki zao na kila mtu anayeonekana adai fedha anaandikwa
jina na kufukuzwa ili wawachukue wafanyakazi wapya.
“Tunaiomba
serikali iwachukulie hatua hii kampuni pamoja na wachina wao kwani sisi
tumefanya kazi kwa zaidi ya muda wa miaka mitatu mfululizo lakini
tulichoambulia ni kufukuzwa kazi huku mafao yetu tukikosa,” alisema William.
Hata
hivyo, meneja wa mgodi huo Elisante Forget alisema wachimbaji hao walikuwa
vibarua wao na siyo wafanyakazi wa kampuni yao ya G and M mining Co Ltd, kwani
hawana mkataba nao wowote wa kuwapa ajira.
Forget
alisema waliandika barua Wizara ya Nishati na Madini ya Desemba 29 mwaka jana
ya kusimamisha shughuli zote za uendeshaji wa mgodi kutokana na kampuni kukosa
fedha za kufanyia kazi hadi hapo watakapopata fedha.
“Hao
wanaodai walikuwa wafanyakazi wetu hatuwatambui na hawatudai fedha zozote, kwani
sisi baada ya kuanza tena shughuli zetu, tulitangaza nafasi za vibarua wapya na
ndiyo hawa ambao wanafanya kazi hivi sasa,” alisema.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa soko la kitalu D John Njau alisema mara nyingi
wamiliki wa migodi huwaeleza wafanyakazi wao kuwa hawana uwezo wa kuwapa fedha zaidi
ya huduma za chakula, malazi na matibabu pindi wakiugua.