Wakazi wa Kijiji cha Loiborsoit A, Kata ya Emboreet Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara, wamemuomba Rais John Magufuli kumwagiza Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi William Lukuvi awanyan'ganye vigogo
waliojimilikisha bila uhalali wa zaidi ya ekari 26,164.5 za mashamba pori ya
kijiji hicho ilihali wananchi wengi wa eneo hilo wamekosa hata ekari moja ya
shamba kwa ajili ya kulima.
Inadaiwa kuwa, baadhi ya vigogo na kiongozi mmoja wa wilaya
hiyo wa chama cha kisiasa wamejimilikisha ardhi kwa kugushi nyaraka na kumiliki
ekari 8,000 mwingine ekari 6,000 na mwingine ekari 4,000 huku vijana wengi wa
eneo hilo wakikosa sehemu za kujishughulisha kwa kilimo.
Akisoma risala kwenye sherehe za kimila za jamii ya wamasai
wakati wa kusimikwa kuwa wazee na kuvuka rika la Irkiponi, mmoja kati ya wakazi
hao Haiyo Mosson alisema watu hao walipora ardhi yao na kujimilikisha bila
kuiendeleza.
Mosson alisema wanamuombea Rais Magufuli kumwagiza Waziri
Lukuvi afike katika eneo hilo kwa ajili ya kuyarudisha mashamba hayo ya
wananchi yaliyoporwa na wajanja wachache wenye tamaa ya ardhi.
Alisema watu hao walijimilikisha na kujiongezea ukubwa wa
mashamba pori hayo huku wakilindwa kupitia nyadhifa zao na watawala wachache
wanaowaunga mkono.
"Wakati wa ujana wetu tulijaribu kuyarudisha mashamba
pori tukishirikiana na serikali ya kijiji japo hatukufanikiwa kwa asilimia
kubwa hivyo tunawasihi vijana wa rika ambalo tunawakabidhi madaraka rasmi leo
hii wajitahidi kuyaenzi na kuyaendeleza yote tuliyoyapigania," alisema
Masson.
Mmoja kati ya waliosimikwa kuwa wazee kwenye sherehe hiyo,
Lee Shinini alisema wananchi wanatambua kuwa suluhishho la tatizo hilo ni kauli
ya Rais Magufuli ndiyo itakayonusuru ardhi yao kuporwa hivyo wanamuomba atengue
umiliki wa vigogo hao waliopora ardhi ya wananchi.
"Tuliona kule Bagamoyo mkoani Pwani hivi karibuni Rais
Magufuli aliwarudishia wananchi ardhi yao waliyokuwa wanaililia kwa muda mrefu
na kupitia fursa hiyo tunaomba atutimizie na sisi wananchi wa kijiji cha
Loiborsoit A," alisema Shinini.
Alisema baadhi ya vigogo hao walitumia nafasi ya vyeo na
madaraka yao, kuwapora ardhi wananchi wanyonge wa eneo hilo lakini wanatambua
suala hilo litahitimishwa kwa kuwanyang'anya na kuwarudishia wananchi wa Kijiji
cha Loiborsoit A.

Diwani wa kata ya Emboreet Christopher Ole Kuya alisema ana
imani kubwa na serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kuwa ni sikivu hivyo
suala hilo litatekelezwa na hatimaye wananchi wa eneo hilo kupatiwa ardhi
yao.
"Kauli mbiu yake ya hapa kazi tuu itashindwa
kutekelezwa na vijana kwa sababu ya masetla wachache waliopora ekari 26,164.5
na kuwakosesha eneo la kulimia nguvu kazi ya Taifa wanaotegemea kunyanyua maisha
yao kupitia kilimo," alisema Ole Kuya.
Alisema kijiji cha Loiborsoit A ni kidogo lakini vigogo hao
wamejimilikisha ardhi hiyo ila kupitia Rais Magufuli, wananchi wataweza
kurudishwa maeneo yao na kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo yao na jamii nzima
kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment